Mgeja kuhudhuria mechi ya kuipongeza Taifa stars kufuzu Afcon
September 12, 2023, 11:26 am
Khamis Mgeja licha tu ya kuwa mdau mkubwa wa michezo nchini amekuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha michezo nchini hasa kwenye masuala mazima yanagusa maslahi mapana ya wananchi na taifa kwa ujumla ambapo amekuwa akiunga mkono timu mbalimbali kwa michango na kuzisaidia pindi zinapokwama ikiwa kwa sasa anasimamia kituo cha Kahama United Sports Academy (KUSA).
Na Paschal Malulu-Kahama
Mwenyekiti mstaafu wa chama cha soka Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) Khamis Mgeja amealikwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa kusheherekea na kuipongeza timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) baada ya timu hiyo kufuzu michuano ya mataifa ya Africa (Afcon).
Mgeja amealikwa kushuhudia mchezo baina ya timu ya vijiji viwili hasimu katika Kata ya Kilago Manispaa ya Kahama ambapo mchezo huo utakuwa kati ya timu ya Nyanhembe Fc dhidi ya timu ya Ngudu FC.
Akithibitisha mualiko huo Khamis Mgeja amesema hatua hiyo ni fursa kubwa ambayo inatoa hamasa na kuonesha uzalendo kwani timu ya taifa inapofuzu wananchi wake hufurahi hivyo hana budi kuhudhuria ili kuendelea kuwaunga mkono mashabiki na wadau wa michezo.
Amesema binafsi anaipongeza taifa Stars kufuzu katika michuano hiyo itakayofanyika nchini Ivory Coast mwezi Januari 2024 hivyo anachoamini yeye kile kinachoenda kufanywa na wananchi wa Kata ya Kilago kinapaswa kuigwa kwani ni timu moja tu inayowaunganisha watanzania ambayo ni timu ya taifa.
Aidha katika mchezo huo wa Nyanhembe FC dhidi ya Ngudu FC utapigwa Jumatano hii Septemba 13, 2023 umedhaminiwa na Mnyama Nzumbi ambapo mbali na mchezo huo sherehe kubwa itafanyika ya pongezi kwa Taifa Stars kufuzu Afcon.