Moto wateketeza mabweni shule ya Mingas, wanafunzi wanusurika kifo
September 6, 2023, 1:27 pm
Na Paul Kayanda-Kahama
Moto mkubwa uliozuka katika shule ya msingi Mingas uliopo katika eneo la Mayila mtaa wa Nyihogo Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga, umeteketeza mabweni yote ya shule hiyo huku wanafunzi wakinusurika baada ya kuokolewa na jeshi la zima moto na uokoaji la wilayani humo pamoja na ushirikiano mkubwa wa makundi ya wananchi.
Licha ya wanafunzi kulazimika kulala katika madarasa ya shule hiyo, jeshi hilo limepongezwa na wananchi kwa kutambua wajibu wao na kuonesha juhudi hizo kwa kutekeleza zoezi la uokoaji hasa baada ya kutua katika eneo la tukio haraka licha ya maji kuisha na mabweni hayo kuendelea kuteketea baada ya jeshi hilo kurudia maji mengine.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo imetokea Septemba 5 majira ya saa 12 kuelekea saa moja jioni huku chanzo cha tukio hilo kikidaiwa kuwa ni jenereta lililokuwa likitumika katika mabweni kutokana na hukuwa na umeme kwenye eneo hilo kutwa nzima.
Shuhuda wa kwanza kufika katika eneo hilo, Kidahi Njige alisema kuwa kama jirani wa karibu na shule hiyo aliona moshi ukifuka kwenye mabweni na kuchukulia ni hali ya kawaida pengine wanafunzi wanafanya usafi kwa kuchoma takataka lakini moshi ulizidi na kuamua kusogea ndipo akabaini kuwa ni mabweni ya wanafunzi wanateketea ndipo alipowaamuru jamaa aliokuwa nao na kufika kwenye eneo la tukio.
Alisema kuwa haraka sana waliita jeshi la zimamoto huku wao wakiomba msaada kwa watu wengine ambao walifika na kuanza kuokoa watoto waliokuwa ndani ya mabweni hayo pamoja na vyombo vya wanafunzi hao, Magodoro, masanduku pamoja na nguo zao na kuongeza kuwa kitu ambacho hakijaokolewa ni pamoja na vitanda pamoja na vitu vingine muhimu vimeteketea kutokana na gari la zima moto kuondoka kufuata maji mengine.
“Kwa kweli tunawapongeza jeshi la zima moto na uokoajji kwa kuwahi lakini walifeli vitu vikateketea baada ya kuja na maji machache na vitu vingi viliteketea baada ya gari kuondoka eneo la tukio na ili kufuata maji mengine, kweli moto ulikuwa mkubwa pamoja na wananchi kuwa wengi na cha kumshukuru Mungu ni kwamba tuliokoa watoto na hakuna vifo wala majeruhi,” alisema Shuhuda huyo.
Aidha shuhuda huyo alisema kuwa kutokana na hali hiyo moto huo uliteketeza pia madaftari ya wanafunzi pamoja na nguo zao huku mashuhuda wengine wakisema kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na jeshi la zimamoto na uokoaji wawe wanafika kwenye matukio ya uokozi kwa wakati kama walivyofanya leo wakiwa wamekamilika vifaa kwaajili ya kazi hiyo kwani maji yangekuwa mengi shule isingepata hasara.
Hata hivyo, Mkuu wa Jeshi la zima moto na uokoaji Wilaya ya Kahama, Mkaguzi Edward Selemani alisema kuwa moto huo ulikuwa mkubwa na umeteketeza vitu vingi na kabla ya maji kuisha walipambana nao mpaka ukazima.
“Katika zoezi hilo hakuna athari iliyojitokeza kama kwa wanafunzi kama vifo tofauti na vitanda na mabweni hayo kuteketea, watoto wote nwaliokolewa na jeshi hili kwa kushirikiana na wananchi lakini pia hasara iliyopatikana pamoja na chanzo cha ajari havijafahamika tutajilidhisha kwanza kisha tutatoa taarifa siku nyingine,” alisema Selemani mkaguzi wa jeshi la zimamoto na uokoaji Wilaya ya Kahama.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Nyihogo Said Mitimingi alikili kutokea kwa ajari hiyo huku akisema chanzo kitafahamika tu wananchi wasiwe na wasi wasi, na kusema huwa hakuna aliyejeruhiwa katika ajari hiyo huku akiwaomba wananchi wazidi kuwa na ushirikiano kama huo.