Tanroads yawakosha wananchi ujenzi wa barabara Shinyanga
September 5, 2023, 12:16 pm
Na Marco Maduhu – Kahama
WANANCHI wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga,wamepongeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani humo, kwa ujenzi wa miundombinu imara ya Barabara, ambayo imekuwa kichocheo kikubwa cha uchumi,pamoja na akina mama wajawazito kuwahi kufika kwenye huduma za afya.
Wamebainisha hayo leo Septemba 4,2023 wakati wakizungumza na Waandishi wa habari,walipofanya ziara kutembelea baadhi ya miundombinu ya Barabara ambayo imetekelezwa na TANROADS katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama.
Miundombinu ya Barabara ambayo imetembelewa ni Mwabomba, Nonwe,Ulowa na Igombe Liver Barabara ambayo ni mpya inayounganisha Ushetu na Tabora yenye urefu wa Kilomita 25.
Baadhi ya Wananchi ambao wametekelezewa Miundombinu ya Barabara hizo akiwemo George Sengerema ambaye ni Dereva wa Magari, amesema awali barabara zilikuwa mbovu hazipitiki, na walikuwa wakiharibu vyombo vyao ya moto pamoja na kupata ajali za mara kwa mara.
Amesema wanaishukuru Serikali kupitia TANROADS, kwa kutengeneza barabara hizo ambazo zilikuwa Korofi,ambapo kwa sasa zipo imara na hakuna tena changamoto za ajali wala kuharibu Magari yao.
“Barabara hizi awali zilikuwa mbaya sana hata kumpitisha Mjamzito ilikuwa Tabu mashimo kila Mahali, lakini sasa hivi tuna tereza tu kama tupo kwenye lami vile, tunaipongeza Serikali kwa ujenzi wa Barabara hizi,”amesema Sengerema.
Naye Amosi Mataba mkazi wa Kaliua mkoani Tabora, ameishukuru TANROADS kwa ujenzi wa Barabara mpya ya Ushetu- Tabora, ambayo kwa sasa bado ipo kwenye matengenezo, kwamba itawasaidia katika shughuli zao za kiuchumi.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS mkoani Shinyanga Mhandisi Mibara Ndirimbi, amesema katika mwaka wa fedha (2022/2023) kwamba kilitengwa kiasi cha fedha Sh.bilioni 15 kwa ajili ya utengenezaji wa miundombinu ya Barabara mkoani humo.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Mibara Ndirimbi.
Amesema pia katika mwaka wa fedha (2023/2024) kimetengwa tena kiasi cha fedha Sh.bilioni 13.8 kwa ajili ya matengezo ya Barabara, na kubainisha katika barabara hiyo mpya ambayo inatoka Ushetu kuunganisha Tabora kwamba hadi kukamilika kwake pamoja na ujenzi wa daraja itagharimu bilioni 3.2.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuitunza miundombinu hiyo ya Barabara, na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kando ya barabara, pamoja na madareva kuacha kupakia mizigo yenye uzito uliopitiliza na kuharibu barabara.