Ilindi waomba kata kupunguza safari ndefu kwenda Zongomela
August 21, 2023, 6:08 pm
Mwenyekiti wa mtaa wa Ilindi kata ya Zongomela Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Dogo Mheziwa, ameliomba baraza la madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kuhalalisha mtaa wa Mwime ya Ilindi kuwa kata inayoweza kujiendesha yenyewe ili kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kwenda Zongomela kwa ajili ya kupata huduma.
Mheziwa amesema kuwa idadi ya watu katika mtaa wake inazidi kuongezeka hivyo serikali kupitia baraza la halmashauri madiwani hao waketi na kuweza kutoa baraka zao ili mtaa huo kuwa kata hali ambayo itapunguza mzigo kwa wananachi pamoja na serikali hiyo ya mtaa kutumia gharama kubwa kwenda kufuata mhuri kwa ajili ya huduma za wananchi.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa wananchi wa Mwime wanapata usumbufu mkubwa kuruka Kata ya Mhungula kwenda Zongomela ambako ndiko makao makuuu ya Kata kwenda kupata huduma stahiki hususani masuala ya utatuzi wa migogoro mbalimbali.
Mwenyekiti huyo ameyasema leo alipokuwa akizungumza na mtandao huu ofisini kwake leo Agost 21,2023 na kutumia mwanya huo kuliomba baraza hilo liangalie namna ya kuwasaidia wananchi wa Mwime ya Ilindi kwa kuwasogezea huduma ya Kata karibu.
“Kumekuwa na changamoto ya kufuatilia Mhuri huko Katani ukilinganisha hali ya uchumi kwa wananchi wetu, kutoka hapa mpaka Zongomela makao makuu ya Kata gharama ni shilingi 3000, na kurudi vile vile,” amesema Dogo Mheziwa Mwenyekiti wa Mtaa.
Amesema kuwa kila kitu wamekidhi mtaa wa ilindi kwamba wanashule tatu za msingi Sekondari pamoja Zahanati kwa mana hiyo kuna haja ya kutupatia Kata kulingana na idadi ya watu na Jioglafia yenyewe.