WAHARIRI WAPIGWA MSASA UANDISHI WA HABARI ZA SENSA
June 16, 2022, 5:54 pm
Na Paschal Malulu-Iringa
Kuelekea kwenye zoezi la sensa ya watu na makazi nchini Tanzania, wananchi wametakiwa kujiandaa kuhesabiwa kwa ajili ya maendeleo ya taifa kwa kuandaa taarifa sahihi.
Hayo yamesemwa na mtaalam wa idadi ya watu, Bi. Hellen Siriwa katika mafunzo kwa wahariri wa vyombo vya habari (redio Jamii) yalioandaliwa na taasisi ya Tanzania Development Information Organization (TADIO) yanayofanyika mkoani Iringa katika chuo kikuu cha Mkwawa University katika Manispaa ya Iringa ambayo yatafanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia leo Juni 16-17, 2022.
Amesema zoezi la sensa ya watu na makazi litaisaidia serikali kuwahudumia wananchi wake kwa kutambua idadi na uhitaji wa huduma inayopaswa kupelekwa kwa haraka kutokana na wingi wa wakazi wa eneo hilo hivyo wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu kwa kutoa idadi kamili ya watu.
Bi. Siriwa amesema zoezi la sensa linatarajiwa kuanza usiku saa sita na dakika moja Agosti 23, 2022 katika nyumba za kulala wageni, wasafiri ambao watakuwa katika vituo vya mabasi, viwanja vya ndege, maeneo ya wavuvi na maeneo mengine ambayo sio sehemu za familia au nyumbani.
Amesema katika maeneo hayo watu wote watakaohesabiwa watapewa karatasi maalum ambayo itawatambulisha kuwa amehesabiwa ili kuepusha kurudiwa kuhesabiwa endapo karani wa zoezi hilo atafika nyumbani kwake tayari amefika.
Nao wahariri wa vyombo vya habari nchini wa redio Jamii wameomba wahudumu wa nyumba za kulala wageni kupatiwa elimu ya kutosha ili kupata taarifa za watu zilizosahihi.
Kwa upande wake, mtaalam wa kukusanya na kusambaza masuala ya kijiografia, Mgambi Benedict amesema zoezi la sensa ni muhimu kwa taifa kwani litasaidia kujua maeneo ambayo hayapaswi kupelekewa huduma fulani na yanahitaji kupeleka huduma nyingine tofauti na ambavyo inafanyika hivi sasa kwani kwa sasa serikali inakadiria baadhi ya miradi ya maendeleo.
Hata hivyo sensa ya watu na makazi inatarajiwa kufanyika mwezi Agosti 23, 2022.
MWISHO