Wanaume chanzo cha ukatili wa kijinsia
September 28, 2021, 8:36 pm
Imeelezwa baadhi ya wanaume ndio chanzo kikubwa cha ukatili wa kijinsia katika jamii kutokana na kutokua tayari kupokea mabadiliko ya kupinga vitendo vya ukatili wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu mradi wa MWANAMKE AMKA Joyce Michael wakati akizungumza kwenye Kikao cha siku moja iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa kupinga ukatili wa kijinsia katika ukumbi wa Ghama hotel wilayani humo.
Amesema wanaume wamekua na mifumo dume ambayo inasababisha mila na desturi kandamizi, kushindwa kubadilika na tamaa ambayo inapelekea vitendo vya ukatili.
Kwa upande wao wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia Mkoani humo wamesema imeonekana wao ndio chanzo kikubwa kinachopelekea ukatili wa kijinsia na kuwepo kwa mifumo dume hivyo elimu iendelee kutolewe mara kwa mara katika jamii.
Kwa upande wake afisa maendeleo kata ya Ngogwa, Ester Sanga ameshauri kupanua wigo wa kutoa elimu hususani shule za sekondari na msingi kuwaaalika walimu wa kiume na kuwapa elimu kwa sababu imeonekana mashuleni ndio chanzo cha ukatili wa kijinsia.
Warsha hiyo ya wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia imehusisha madereva pikipiki maarufu bodaboda,wananchi wa kawaida, viongozi wa serikali za mitaa na wadau mbalimbali wa halmashauri ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga