Machinga walionyang’anywa Matunda yao warejeshewa na Mkuu wa Wilaya
July 19, 2021, 8:00 pm
Kufuatia kukamatwa kwa wafanyabiashara wa matunda wa soko la Mkulima na kuonesha Migambo wakigombana na wauza matunda hao mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga ametatua Mgogoro huo.
Akiongea na wafanyabiashara wadogo katika stendi ya CDT mkuu wa Wilaya, Festo Kiswaga amesema amewasamehe wauza matunda wote waliokamatwa na migambo na kupelekwa polisi pamoja na matunda yao huku akisema serikali inathamini wamachinga hivyo kawasihi kufanya kazi kwa kufuata Sheria.
Pia amemtaka mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Anderson Msumba kuangalia matunda ya wafanybiashara hao kama kuna kasoro imejitokeza awasaidie ili waendelee na biashara zao kama kawaida pamoja na hayo pia amewaasa migambo kuacha kujichukulia sheria mikononi kwa kuwa jukumu hilo ni kosa kisheria hivyo waache mara moja.
Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri ya Kahama, Anderson Msumba amemuahidi mkuu wa Wilaya kuwa ataendelea kuwatumikia wafanyabiashara bila kujali itikadi za vyama vyao na dini wala kabila huku akiwaasa watu wajitokeze kuunda vikundi ili kuchukua mikopo kwani tayari halmashauri imetenga bajeti ya Zaidi ya bilioni moja.
Kwa upande wao wafanyabiashara maarufu “machinga” wauza matunda waliokuwa wamekamatwa wamemshukuru mkuu wa Wilaya na kufutwa kesi na kurejeshewa matunda yao kwani wanafamilia zinazo wategemea kupitia matunda hayo.