Wasimamizi uchaguzi mdogo watakiwa kuzingatia matakwa ya tume ya uchaguzi na maadili yake.
April 19, 2021, 3:02 pm
Washiriki wa semina ya mafunzo ya uchaguzi mdogo katika halmashauri saba nchini wametakiwa kujitambua, kujiamini, kufuata na kuzingatia katiba ya nchi na maadili ya tume ya uchaguzi na sheria zake.
Hayo yamesemwa na kamishna wa tume ya taifa ya uchaguzi nchini Balozi Omary Ramadhan Mapuri katika ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Kahama wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa washiriki wa semina ya wasimamizi wa uchaguzi mdogo nchini.
Pia Balozi Mapuri amewataka washiriki wote waliofika kwenye mafunzo hayo kwa pamoja kujadili namna ambavyo watakavyoweza kufanikisha chaguzi ndogo zitakazofanyika katika halmashauri zao ili kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza.
Mafunzo hayo yatafanyika kwa siku tatu ambayo yameanza leo April 19 hadi April 21 mwaka huu kwa kuhudhuriwa na maafisa wa halmashauri saba za Nzega, Uyui, Igunga za mkoani Tabora, Chato, Geita za mkoani Geita, Kongwa ya mkoani Dodoma na Msalala ya mkoani Shinyanga.
Hata hivyo tume ya taifa ya uchaguzi nchini ilitangaza Mei 16 mwaka huu chaguzi ndogo zitafanyika katika halmashauri 17 zenye jumla ya kata 18 kutokana na sababu mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo vifo na baadhi ya wagombea kuhama vyama vyao.