Kambi za kujitambua kujithamini na kujiamini ziwe endelevu.
22 June 2021, 7:38 pm
Rai imetolewa kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na shule za sekondari kujenga msingi endelevu wa kuwa na kambi za watoto wa kike kipindi cha likizo lengo ikiwa ni kuwaweka pamoja ili waweze kujifunza masomo mbalimbali ikiwemo lugha ya kiingereza na elimu mbalimbali jambo litakalowasaidia kujitambua, kujithamini na kuwa na muda zaidi wa kujenga uelewa wa masomo yao.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Awali na Msingi OR-TAMISEMI Bi. Suzan Nyarubamba wakati wa ufunguzi wa kambi ya mafunzo kwa mtoto wa kike Kilosa iliyoandaliwa na Mbunge wa jimbo la Kilosa ambapo amesema kupitia kambi hizo anaamini zitaleta mabadiliko kwa mtoto wa kike na kumtengenezea mazingira mazuri kielemu na kujitambua huku akiagiza kuanzishwa kwa kambi za jinsia mashuleni zitakazokuwa zikifundisha stadi za maisha, utunzaji wa mazingira, elimu ya ukimwi na masomo mengineyo.
Aidha ametaka kufanyiwa marekebisho kwa sheria kandamizi kwa mtoto wa kike ambazo zinakwamisha kufikiwa kwa ndoto za mtoto wa kike huku akiwataka waheshimiwa madiwani kuhimiza wananchi kuibua watoto wenye mahitaji maalum ili waweze kupata elimu na stahiki zao.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kilosa ambaye pia ni Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba Kabudi amesema kambi hiyo inayofanyika shule ya sekondari Dakawa inajumuisha wanafunzi wakike 220 toka shule za sekondari 22 za kata katika jimbo la Kilosa inalenga kuhamasisha wasichana katika shule za sekondari kujitambua, kujithamini na kujiamini pamoja na kuwaunganisha wasichana kuainisha fursa na changamoto zilizopo kijamii, kiuchumi na kitaaluma.
Kabudi amesema kupitia kambi hiyo yenye kauli mbiu ya #Msichana wa Kilosa Timiza Malengo kwa Ustawi wa Kilosa Yetu watajifunza kuhusu stadi za maisha, elimu ya ukimwi, masomo ya sayansi na kiingereza, historia ya nchi pamoja na safari ya mafunzo katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine(SUA) huku akisema kambi hizo zinatarajiwa kufanyika kila mwaka na kwamba kwasasa zimeanza na wasichana ambao kwa asilimia kubwa huathirika na changamoto mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni, ndoa za utotoni na changamoto nyinginezo ambapo kwa siku za baadae kambi hizo zitahusisha na wanafunzi wakiume.
Sambamba na hayo amesema Serikali ina mpango wa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule za kata na kwamba kupitia mpango wa kuboresha elimu inakusudia kuboresha elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ikiwemo shule ya msingi Mazinyungu.