Radio Jamii Kilosa

WEO Kilosa washauriwa kusimamia vema miradi ya maendeleo

12 November 2024, 6:59 am

Kushoto Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Ndg Michael John Gwimile akiwa katika kikao kazi

Watendaji wa kata kutambua kuwa jukumu la kusimamia miradi linaenda sambamba na kuwajibika kwa ufanisi wa vyanzo vya mapato vya halmashauri.

Na Asha Madohola

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg Michael John Gwimile, akizungumza katika kikao kazi cha watendaji wa kata kilichofanyika 11 Novemba 2024 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, aliwataka watendaji hao kusimamia kwa umakini na ufanisi miradi yote ya maendeleo katika maeneo yao.

Amesema watendaji wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa wakati na viwango vinavyotarajiwa ili kufanikisha lengo la serikali la kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Watendaji kata wakifuatilia kikao kazi

Mkurugenzi Mtendaji amesisitiza kwamba usimamizi thabiti wa miradi ni msingi wa kuleta mabadiliko chanya kwa jamii, huku akieleza kuwa watendaji wanapaswa kuibua na kuzitolea taarifa changamoto zinazojitokeza mapema.

“Changamoto zinazotokea kwenye miradi lazima zifahamike mapema ili hatua zichukuliwe mara moja na kazi ya mtendaji sio tu kuratibu miradi, bali kuhakikisha inafikia malengo yake kwa viwango vilivyokusudiwa, tunataka kuona kuwa fedha za umma zinatumika kwa manufaa ya kweli kwa wananchi na si vinginevyo” alisema Mkurugenzi Mtendaji.

Akiendelea na maelekezo yake, amesema ni muhimu kwa watendaji kuainisha na kutambua vyanzo vya mapato vilivyopo katika maeneo yao ambavyo bado havijafikiwa au kutumiwa kikamilifu na serikali.

“Lazima tuwe wabunifu katika kutafuta na kuongeza mapato ya halmashauri kwa kutumia vyanzo vyote vilivyopo, na mapato hayo ni muhimu kwa kuboresha huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wananchi” alieleza Mkurugenzi Gwimile.

Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa halmashauri George Lazaro Burton aliwataka watendaji wa kata kuhakikisha mapato yanayokusanywa na vijiji yanaingizwa benki ili kupunguza mianya ya uvujaji wa mapato na kuongeza uwazi katika ukusanyaji huo.

Aliwahimiza pia kusimamia wenyeviti wa vijiji kuwajibika kwa kuitisha mikutano ya mara kwa mara kwa mujibu wa sheria, hatua ambayo inasaidia wananchi kufuatilia matumizi ya mapato yao.

Afisa huyo aliwahimiza watendaji kuhuisha sheria ndogondogo za vijiji ili ziwasaidie kuwaongoza na kuhakikisha matumizi sahihi ya mapato ya vijiji kwa manufaa ya wananchi.

Kikao hicho kilimalizika kwa watendaji wa kata kuonesha nia ya kuyatekeleza maagizo yaliyotolewa, wakiapa kufanya kazi kwa bidii na kujituma katika kuhakikisha miradi ya maendeleo na ukusanyaji wa mapato unafanyika kwa mafanikio na matokeo yanayoonekana.