Radio Jamii Kilosa

Habari za uongo kikwazo kipindi cha uchaguzi

24 October 2025, 6:16 pm

Mgombea ubunge jimbo la Mikumi kwa tiketi ya chama cha Act Wazalendo Kasela Hassan Mdachi. Picha na mtandaoni

Kuelekea uchaguzi mkuu, kumekuwa na ongezeko la habari za uongo na uzushi zinazosambazwa hasa kupitia mitandao ya kijamii. Habari hizi huwalenga wagombea, vyama vya siasa na taasisi mbalimbali kwa lengo la kupotosha umma, kuchafua sifa za watu au kuvuruga amani.

Na Asha Madohola

Katika kipindi cha Mambo Mseto kinachorushwa na Redio Jamii Kilosa, mada iliyojadiliwa ni: “Kwa nini habari za uongo/uzushi mara nyingi huzushwa kipindi cha uchaguzi na athari zake katika jamii”.

Mada hii imechambuliwa kwa kina kwa njia ya simu na mgeni mgombea ubunge jimbo la Mikumi kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Ndugu Kasera Hassan Mdachi ambapo alisema kuwa kipindi cha uchaguzi kimekuwa maarufu kwa kusambaa kwa taarifa zisizo za kweli ambazo mara nyingi hulenga kuharibu taswira ya wagombea au kupotosha wananchi.

Mgombea huyo alitoa rai kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha inasimamia kwa ukaribu taarifa zinazosambazwa mitandaoni na kuweka uthibiti madhubuti kwa wale wanaosambaza uzushi huku akisisitiza kuwa, kuna haja ya kuwa na mifumo ya kisheria inayowabana wanaotumia mitandao vibaya kwa kusambaza taarifa za uongo, hasa katika kipindi nyeti kama cha uchaguzi.