Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
7 October 2025, 6:59 am

Zoezi la kampeni limeendelea katika Jimbo la Kilosa ambapo wagombea kutoka vyama mbalimbali wanaendelea kunadi sera zao kwa wananchi, wakiahidi kuboresha huduma za jamii kama afya, elimu, maji na kutatua changamoto za wakulima na wafugaji, huku wakiomba ridhaa ya kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Na Aloycia Mhina
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kilosa kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Hassan Mbaruku, aliahidi kuwa iwapo atachaguliwa kuwa mbunge, atahakikisha anasimamia ujenzi wa vituo vya afya na zahanati katika kata ambazo bado hazijafikiwa na huduma hizo muhimu wilayani Kilosa.
Alitoa kauli hiyo Oktoba 4, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya soko la mjini, Kata ya Mbumi, ambapo alisisitiza kuwa lengo lake ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya kwa ukaribu, jambo ambalo litapunguza gharama na muda wa kufuata huduma mbali.
Sambamba na hilo, Mbaruku ameahidi kuanzisha viwanja vya michezo katika kila kata ya jimbo hilo, akieleza kuwa michezo ni ajira kwa vijana na pia huimarisha afya. Aidha, ameeleza mpango wake wa kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kuanzisha maeneo maalumu ya kuzalisha nyasi endelevu kwa ajili ya mifugo.

Kwa upande wake, Naibu Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, aliwanadi wagombea wa chama hicho na kuwasihi wananchi wa Kilosa kuwachagua viongozi bora wenye maono ya kweli ya kuleta maendeleo, akisema kiongozi bora ni yule anayeacha alama ya mafanikio katika jamii.
