Radio Jamii Kilosa

Mgombea CUF: Nitapigania haki za wenye ulemavu

21 August 2025, 5:22 pm

Mgombea Ubunge Jimbo la Kilosa Kupitia chama cha Wananchi (CUF) Ndg. Silas Ramadhani Kassao akiwasili katika ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kilosa na Mikumi ili kuchukua fomu ya uteuzi. Picha na Asha Madohola

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) zoezi la uchukuaji wa fomu za uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani yameanza tarehe 14 Agosti, 2025 hadi tarehe 27 Agosti, 2025 ambapo wagombea wa vyama vya siasa waliopitishwa na vyama vyao kuingia katika kinyang’anyiro hicho katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika 29 Oktoba 2025.

Na Asha Madohola

Mgombea ubunge wa Jimbo la Kilosa kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Ndg. Silas Ramadhani Kassao, leo amechukua fomu ya uteuzi katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo ya Kilosa na Mikumi, Ndg. Joseph Kapere. Hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika 29 Oktoba 2025.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Kassao amesema amepata idhini ya chama chake kugombea nafasi hiyo ili kutekeleza sera za CUF kwa vitendo, hasa katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa Kilosa. Miongoni mwa vipaumbele vyake ni kuongeza ajira kwa vijana, kuboresha maisha ya wakulima na wafugaji, pamoja na kutokomeza tatizo la wanyama waharibifu wa mazao.

Mgombea kupitia chama cha wananchi CUF Silas Kassao akisaini fomu ya uteuzi

Amesisitiza kuwa ana dhamira ya kuleta mabadiliko chanya katika jimbo hilo kwa kuimarisha fursa za kiuchumi na kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki zao za msingi bila ubaguzi. Ameahidi kuwa mwakilishi wa wananchi wote bila kujali makundi au tofauti zao.

Sauti ya Mgombea Silas Kassao akizungumza vipaumbele vyake

Silas Kassao ni Afisa Sheria pia ni Katibu wa Mkoa wa Morogoro wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), na anasema uzoefu wake katika kutetea haki za makundi maalum utamsaidia kuwa mbunge wa wote atakayesikiliza na kushughulikia kero za wananchi kwa ukaribu.

Mgombea Ubunge Jimbo la Kilosa kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Ndg. Silas Ramadhani Kassao akikabidhiwa fomu ya uteuzi na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kilosa na Mikumi Ndg. Joseph Kapere