Radio Jamii Kilosa
Radio Jamii Kilosa
14 May 2025, 9:40 pm

Wananchi wamepatiwa wasaa wa kushiriki kuhakiki na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapigakura nchini ili waweze kutumia haki ya msingi ya kikatiba ya kupiga kura kwa kumchagua kiongozi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Na Asha Madohola

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeanza rasmi awamu ya pili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.
Katika mafunzo yaliyofanyika leo katika ukumbi wa FDC Ilonga, wilayani Kilosa, Mkurugenzi wa Tume hiyo, Ramadhani Kailima, aliwataka watendaji wa uboreshaji ngazi ya Halmashauri kuzingatia uadilifu na uaminifu katika kutekeleza zoezi hilo muhimu.
Kailima alisisitiza kuwa uaminifu ni jambo la msingi katika kuhakikisha kuwa mchakato wa uboreshaji unafanyika kwa uwazi na haki, hivyo kuimarisha imani ya wananchi katika mfumo wa uchaguzi. Aliongeza kuwa zoezi hilo linahusisha kuandikisha wapiga kura wapya, kurekebisha taarifa za wapiga kura waliopo, na kuhamisha taarifa kwa wale waliobadilisha maeneo yao ya makazi.

Kwa upande wake, Afisa Mwandikishaji wa Majimbo ya Kilosa na Mikumi, Betuely Ruhega, alisisitiza umuhimu wa uwazi katika zoezi hilo kwa wananchi. Alieleza kuwa ni muhimu kwa wananchi kufahamu haki zao na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uboreshaji wa daftari ili kuhakikisha kuwa taarifa zao ziko sahihi na wanastahili kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.

Washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo, Oscar Joel na Shania Mohamed walieleza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa kwa kina taratibu na kanuni za uboreshaji wa daftari la wapiga kura.
Aidha alitoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika vituo vya uandikishaji kuanzia tarehe 16 hadi 22 Mei 2025, ili kuhakikisha kuwa taarifa zao ziko sahihi na wanastahili kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.