Radio Jamii Kilosa

Wanawake Kilosa waaswa kugombea nafasi za uongozi

10 September 2024, 12:00 am

Katibu wa Umoja wa Wanawake CCM Wilaya ya Kilosa Bi Joha Dole. Picha na Farida Hassan

Na Farida Hassan

Uoga na kutojiamini zimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea wanawake wengi nchini kushindwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi serikalini.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi UWT Wilaya ya Kilosa Bi Joha Mohamed Dole wakati akizungumza na Redio Jamii Kilosa akiwa ofisini kwake.

Bi Dole amesema kuwa ili kuwa na jamii bora yenye maendeleo inahitajika kuwa na wanawake shupavu ambao watajitokeza kushiriki nyadhifa mbalimbali za uongozi katika jamii zao na taifa kwa ujumla.

Sauti ya Bi Joha Dole

Naye Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi UWT Kata ya Kasiki Bi Marietha Kesi ametoa wito kwa wanawake kuiga mfano mzuri kutoka kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alithubutu na sasa ndiye anaeliongoza taifa.

Kwa upande wake Sada Sadi ambaye ni mwananchi, ameziomba mamlaka zinazohusika na kusimamia upatikanaji wa haki ikiwemo TAKUKURU kuingilia kati tatizo la rushwa ya ngono kwani vitendo hivyo vimekuwa vikirudisha nyuma jitihada za wanawake kushika nafasi mbalimbali za uongozi.