Ujenzi wa barabara za kiuchumi wawakuna wakulima Kilosa
9 April 2024, 3:07 pm
Serikali imedhamiria kwa dhati kumaliza changamoto za miundombinu ya barabara kwa kutengeneza madaraja, mifereji na makaravati wilayani Kilosa kwa kuondoa adha ya usafiri na kuwainua wananchi kiuchumi kwa kuweza kusafirisha mazao yao kuyapeleka kwenye masoko makubwa ambayo yatawaongezea kipato mara dufu.
Na Asha Rashid Madohola
Wakulima wa kata za Mbumi na Magomeni wanaolima katika bonde la Kisaki wamenufaika na mradi wa ujenzi wa miundombinu ya barabara mbili ambapo awali hakukua na barabara maeneo hayo na kusababisha kuzorota kwa shughuli za kiuchumi.
Hayo yamebainika katika ziara ya Mbunge wa jimbo la Kilosa akiwa pamoja na kamati ya siasa ya CCM wilaya ya Kilosa ambao walifika na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo na kuridhishwa na maendeleo ya mradi ambapo wananchi wanaendelea kuzitumia licha ya kwamba hazijakamilika.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata ya hiyo Bi Fatuma Saidi na diwani wa kata ya Magomeni Mchuuzi Limbanga wameishukuru serikali kwa kuwapelekea mradi wa barabara ambapo imeshachongwa umbali wa kilomita moja na wananchi itawanufaisha kiuchumi kwa kuwa wanategemea kilimo kukuza kipato chao.
Aidha ziara hiyo ilifika kukagua mradi wa ujenzi wa mfereji wenye urefu wa mita 450 unaogharimu shilingi milioni 200 ambapo mkandarasi wa mradi kupitia kampuni ya Kupala Works Bi Mary Sanga na Meneja wa Tarura wilayani Kilosa Winston Mnyaga wamesema hali ya mradi inaendelea vizuri changamoto iliyopo na hali ya hewa ya mvua ndio inachelewesha ukamilishaji wa mradi.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Shaban Mdoe alisema ziara hiyo imekua ya mafanikio makubwa kwa kuwa wamekagua na kuziona changamoto ila miradi yote inaendelea vizuri na hivi karibuni wananchi watanufaika na miradi hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Wilfred Sumari alishukuru kata yake kupelekewa mradi wa barabara kuanzia Ilonga hadi Mfuluni na kuomba serikali kuzimalizia kilometa tatu ili ifike Kijiji cha Idete na kuwanufaisha wananchi wa huko.
Hata hivyo wakiwa katika kata ya Rudewa wananchi waliiomba serikali kuwaondolea adha ya barabara ya kutoka Tembeni hadi Peapea kwa kuwa kipindi cha mvua haipitiki huku ng’ombe wakiwa kero katika kuharibu miundombinu hiyo.
Kwa upande wake Mbunge Prof Palamagamba Kabudi aliishukuru serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Hassan kwa kulipatia jimbo la Kilosa fedha nyingi za kuwaletea wananchi miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara na kuwataka wananchi wawe na imani na serikali yao kwa kuwa maendeleo yatawafikia wote.