Halmashauri Kuu ya CCM Kilosa yajipanga kumpongeza Rais Samia
27 February 2024, 10:16 am
Katika kipindi cha miaka mitatu wilaya ya Kilosa ilipatiwa fedha nyingi kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwepo ya sekta ya elimu, afya, maji na miundombinu ambayo utekelezaji wake umetekelezeka katika kata zote chini ya ilani ya chama cha mapinduzi.
Na Asha Rashid Madohola
Wajumbe wa Halmashauri kuu ya ccm wilaya ya Kilosa imeazimia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anafanya kazi nzuri katika serikali kuu anayoiongoza na kwa kuitekeleza na kuisimamia ilani ya chama cha CCM.
Hayo yalisemwa na Katibu wa ccm wilaya ya Kilosa Shaban Mdoe katika kikao cha Halmashauri Kuu Ya CCM cha kusoma na kupitia taarifa za utekelezaji wa ilani ya chama cha CCM kwa mwaka 2020 hadi 2025 na kimeweka maazimio manne ikiwemo la kumpongeza Mhe Rais Dkt Samia kwa kupeleka fedha nyingi wilayani Kilosa pamoja ya kuleta Miradi ambayo inaendelea kutekelezwa.
“Sisi chama na serikali ni damu damu tunaendelea kushirikiana na kudumisha umoja ambapo wanatakiwa kuyatelekeza yale yote walioyaazimia kabla ya kukutana kwenye kikao kijacho kwa kutoa taarifa kwa kamati ya siasa” alisema Katibu Mdoe.
Hata hivyo katibu huyo aliongeza kwakuwapongeza wabunge wa jimbo kilosa na Mikumi kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya kwa kuwaletea wananchi maendeleo na kusimamia vema ilani ya CCM na kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa wamejipanga kwa kuhakikisha wanachukua vitongoji na vijiji vyote.
Wakati wakiwasilisha taarifa kwa wakuu wa idara mbalimbali akiwepo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Joseph Kapele alisema kuwa Halmashauri imeunda kuunda kikosi kazii kufanya ufuatiliaji wa miradi mara kwa mara ili kuleta msukumo wa kukamilika kwa wakati, huku shirika la Tanesco Kilosa wakitoa taarifa ya kuhujumiwa kwa miundombinu.
Awali akitoa taarifa katika kikao hicho cha halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Kilosa Mjumbe ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Kilosa Mhe Prof Palamagamba Kabudi alimshukuru Mhe Dkt Rais Samia kwa kuwapatia majimbo yote mawili fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuwataka wajumbe waungane pamoja ili kuleta mageuzi chanya ya maendeleo na wasisambaratike kwa vuguvugu la uchaguzi.