Waganga wafawidhi Kilosa wasisitizwa kutumia mfumo wa Got-HoMIS
17 November 2023, 2:19 pm
Katika kuboresha huduma bora za afya na kudhibiti upotevu wa mapato katika vituo vya afya na zahanati serikali imevitaka vituo hivyo kuimarisha usimamizi wa utumiaji wa mfumo wa GoT-HoMIS ambao utaleta ufanisi katika masuala ya usimamizi wa dawa,vifaa tiba, pamoja na kutunza kumbukumbu nzuri ya taarifa za wagonjwa watakaofika kupata huduma na kuboresha usimamizi wa mapato ya Hospitali.
Na Asha Rashid Madohola
Waganga wafawidhi kutoka vituo vya afya pamoja na zahanati wametakiwa kuhakikisha wanatekeleza agizo la kununua vifaa stahiki kwa ajili kufunga mfumo wa GoT-HoMIS katika vituo vyao vya kazi hususani katika vituo vya afya na zahanati ambazo hazijatekeleza agizo hilo.
Agizo hilo limetolewa Novemba 16, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Kisena Mabuba wakati wa kikao kazi kilichoshirikisha waganga wafawidhi wa vituo vya afya na zahanati pamoja na wahasibu wa vituo hivyo ambapo alisema kuwa mfumo huo unataunza taarifa za kifedha zinazokusanywa kupitia wagonjwa wasio kuwa na bima za afya na kurahisisha upatikanaji wa takwimu mbalimbali kuhusu wagonjwa waliopata huduma katika vituo hivyo.
“Baada ya kubaini kuwa bado kuna changamoto katika ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mfumo wa GoT-HoMIS kitendo ambacho kinapelekea upotevu wa mapato kila mmoja anatakiwa kutekeleza agizo hilo ili kuondoa changamoto katika ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mfumo wa GoT-HoMIS” alisema Mkurugenzi Mabuba.
Hata hivyo aliwataka watumishi hao kuacha ubinafsi kwa kuhakikisha wanalinda kazi zao kwa kufanya majukumu yao inavyostahiki kwani ni watumishi wa umma ambao wanapaswa kuzingatia uwajibikaji kwa kutoa huduma nzuri kwa watu wanaowahudumia, huku akisisitiza suala la usimamizi wa matumizi sahihi ya fedha za Serikali pamoja na miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.