CCM yaridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa uzio shule ya msingi Mazinyungu
18 July 2023, 12:07 pm
Kupatiwa fedha na serikali katika mradi wa shule ya ujenzi wa uzio katika ya shule ya Mazinyungu unakwenda kuwanufaisha wanafunzi shuleni hapo ambao walikua wanakumbana na adha mbalimbali hususan ya usalama wao wawapo shule kwa kuwa shule hiyo ipo karibu na barabara kuu.
Na Asha Madohola
Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa uzio katika shule ya Msingi Mazinyungu iliyopo katika kata ya Kasiki wilayani Kilosa umeleta mwangaza mpya kwa kuondoa hali ya utoro kwa wanafunzi ambao walikuwa wakitoroka wakati masomo yakiendelea.
Akizungumza Mwalimu Gallan Kajika ambaye ni Mkuu wa Shule ya Mazinyungu mara baada ya kukamilika kwa ziara ya Sekrieti ya CCM ya kata ya Kasiki ambayo ilifika shuleni hapo kukagua mradi wa ujenzi wa uzio unavyoendelea ambapo alisema kuwa imekuwa chachu kwao kwa kuongeza umakini kiutendaji na kuitaka jamii ishirikiane katika kuutunza mradi huo kwani itakua suluhu ya utoro shuleni.
“Serikali iliweza kutupatia fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huu wa shule na tunashukuru tumeusimamia vema na umekamilika na kwa sasa imefikia hatua ya kusimika mageti yakikamilika yatatusaidia katika ulinzi wa wanafunzi hususan kwa utoro” alisema Mwl Kajika
Naye Katibu wa UWT kata ya Kasiki Mareta Alexander Kessy amesema wametembelea mradi huo na kuuona namna unavyoendelea vizuri na kuwashukuru kwa usimamizi mzuri uliofanyika hali unaoleta matumaini mapya kwa watoto kuwa na eneo salama la kujisomea muda wote wa masomo pasipo na kutoroka.
Kwa upande wake Katibu wa CCM tawi la Mazinyungu Kigolo Abdallah Kigolo ameishukuru serikali kwa kuleta fedha shuleni hapo kwa ajili ya ujenzi wa uzio na mradi upo ukingoni kukamilika na kwamba chama kimeridhika na kazi iliyofanyika kwa ufasaha huku akiitaka jamii kuacha kuwatumikisha watoto kazi nyakati za shule.