Zaidi ya shilingi milioni 14 za wananchi kuanza ujenzi wa barabara wa kilomita kumi kijiji cha Mbamba
18 July 2023, 11:19 am
Ukosekanaji wa barabara unachangia kwa kiasi kikubwa kuzorota kwa maendeleo katika maeneo mengi hasa ya wananchi wanategemea kilimo kuwakomboa kiuchumi na wakati mwingine majanga kama vile vifo hutokea hususan kwa akinamama wajawazito kukosa usafiri pindi wanapojitaji kwenda Hospitali.
Na Asha Madohola
Wananchi wa kijiji cha Mbamba kilichopo kata ya Kilangali wilayani Kilosa wameridhia kuchangishana fedha kwa ajili ya kuanza mradi wa ujenzi wa barabara ili kuondokana na changamoto ya ukosekanaji wa barabara ya uhakika inayowakabili kwa muda mrefu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kijiji hicho walisema kuwa hali imekua ngumu kwenye barabara hali inayochangiwa kukosekana kwa maendeleo kwa kuwa wanategemea kilimo lakini usafirishaji wa mazao kupeleka mazao sokoni hakuna kutokana na adha ya barabara hivyo wanauza kwa bei kandamizi na kupelekea kushindwa kujikwamua kiuchumi.
Bi Frola Bura mkazi wa kijiji hicho akizungumza katika mkutano wa hadhara mbele ya diwani wa kata ya Kilangali Mhe Amos Thomas Kusupa alisema kuwa kukosekana kwa barabara inawagharimu gharama kubwa kutumia usafiri wa pikipiki kwenda kutafuata mahitaji muhimu ya kijamii hivyo wamekubaliana kuchangishana fedha ili ujenzi wa barabara uanze ambao ndio itakua chachu ya maeneo katika kijiji chao.
Naye Bw Amos Dominic Kizibo mkazi wa Mbamba alisema maendeleo yanaletwa na wananchi wenyewe hivyo ni wajibu wao kuchangishana fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ambayo itafungua fursa za kibiashara kijijini hapo na wakulima wataweza kuyasafirisha mazao yao kwenye masoko ya nje na itawasaidia kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo.
Hata hivyo Mzee Kassimu Magona alimshukuru Mhe diwani kwa kuwaletea mchakato wa ujenzi wa barabara na kusema ni wakati wa wananchi kuwaunga mkono viongozi pale wanapoamua kuleta nyenzo za uletaji wa maendeleo, huku akiwashauri wafanyabiashara wote wa kijijini hapo kujitokeza kwa wingi na kuchangia fedha za kutosha katika zoezi la ujenzi wa barabara.
“Sisi ambao ni wadau wakubwa ambao ni wafanyabiashara na wafugaji katika kijiji hiki tuungane pamoja kuchangia fedha ili tuharakishe kukamilika kwa haraka ujenzi wa barabara yetu ambayo itakua mkombozi kwetu wananchi kuturahisishia usafiri na maendeleo yataonekana” alisema Mzee Magona
Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Mhe Amos Kusupa aliwashukuru wananchi wa kijiji cha Mbamba kwa kuridhia kuunga mkono jitihada za serikali za kuleta maendeleo na kuamua kushirikiana kuchangishana fedha za michango katika vitongoji vitano vyenye nguvukazi 1337 ambazo zitasaidia kuanza kwa ujenzi wa barabara ambapo itakua fursa nzuri kwa wadau wengine wa maendeleo kujitokeza ili kuwaunga mkono na atahakikisha unaanza mapema.
“Nawashukuru wananchi wangu kwa kukubaliana kuchangia shilingi elfu kumi kwa kila mwananchi hii inaonesha ni kwa namna gani mna uchu wa maendeleo na mimi kama diwani wenu nitahakikisha nashirikiana vyema na serikali kupitia kwa Mkurugenzi na wadau ili waweze kutuunga mkono kwa kutupatia vifaa ila na mimi nitachangia shilingi milioni moja” alisema Mhe Kusupa.
Michango hiyo ya wananchi inayotarajiwa kukusanywa hadi Julai 30 mwaka huu itaanza ujenzi wa barabara hiyo utakayoanzia kijiji cha Mbamba hadi kijiji cha Kivungu wenye urefu wa kilomita kumi.