Radio Jamii Kilosa

Uzinduzi kampeni za uchaguzi wa udiwani CCM Kilosa mgombea akabidhiwa ilani ya chama Magubike

6 July 2023, 4:50 pm

Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa anayewakilisha mkoa wa Morogoro Jonas Nkya. Picha na Yusuph Kayanda

Kutokana na kuachwa wazi katika kata mbalimbali Tanzania bara, Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC ilitangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 14 utakaofanyika Julai 13 mwaka huu na kampeni zilianza tangu Julai mosi hadi Julai 12 mwaka huu.

Wale wote watakaoleta viashiria vya uvunjifu wa amani kwenye kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi serikali ipo macho itawashughulikia hivyo kila mwananchi atumie haki yake ya msingi ya kupiga kura kwa amani na utulivu.

Na Asha Madohola

Chama Cha Mapinduzi CCM wilayani Kilosa kimezindua rasmi kampeni za uchaguzi katika kata ya Magubike ambayo ni mojawapo ya kata 14 kutoka Tanzania bara iliyoingia kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani kufuatia nafasi iliyoachwa wazi baada ya kifo cha aliyekua diwani wa kata hiyo.

Akifungua kampeni hizo za uchaguzi Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa anayewakilisha mkoa wa Morogoro Jonas Nkya alisema kuwa chama kimemteua ndugu Abuu Msofe kuwa mgombea nafasi ya udiwani katika kata ya Magubike na wanaamini wananchi watampigia kura za kutosha kutokana umahiri katika utendaji kazi wake na kama chama wamemuamini.

“Msifanye makosa kwenye kupiga kura nendeni mkape kura za ndio Abuu kwa kuwa ni kijana mchapakazi na asiyekata tamaa kwa kuwa alianza kuomba idhaa ndani ya chama ya kugombea udiwani lakini kura haizikutosha amerudi tena na chama kimempa nafasi basi nanyi mkafanye hivyo ili kuharakisha maendeleo hapa Magubike”alisema Mnec Nkya.

Sauti ya MNEC Jonas Nkya
Mgombea udiwani kata ya Magubike ndg Abuu Msofe

Akiomba idhaa ya kupigiwa kura za ndio diwani mteule kutoka CCM Abuu Msofe alisema kuwa ili maendeleo yapatikane katika kata ya Magubike ni lazima kuwe na mafiga matatu imara ambapo kwa sasa yapo mawili hivyo amewaomba wananchi kumuongeza awe figa la tatu ili aweze kushirikiana vema na Rais Dkt Samia, Mhe mbunge Prof Kabudi ili kutatua changamoto zao.

Sauti ya ndg Abuu Msofe
Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe Shaka Hamdu Shaka

Akizungumza Mkuu wa wilaya ya Kilosa ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa Mhe Shaka Hamdu Shaka aliwataka wananchi kudumisha amani na utulivu kipindi hiki cha uchaguzi na alivikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi chote cha uchaguzi.

“Kilosa ipo salama katika suala la ulinzi na usalama na kuna watu wamedhamiria kufanya vurugu ili waharibu uchaguzi nasema serikali ipo macho na itawashughulikia nende mkapige kura kwa amani na utulivu” alisema Mhe Shaka.

Sauti ya Mhe Shaka Hamdu Shaka
Mbunge wa jimbo la Kilosa Prof Palamagamba Kabudi

Awali akizungumzia miradi inayotekelezwa katika jimbo la Kilosa Mbunge wa jimbo hilo Mhe Prof Palamagamba Kabudi alimshukuru Rais Dkt Samia kwa kuwapatia fedha nyingi ambazo zimesaidia kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa majengo ya kituo cha afya Magubike ambacho kilikua na majengo chakavu ya tangu mwaka 1966.

Sauti ya mbunge Prof Palamagamba Kabudi