Wakulima Lumuma wanufaika elimu uhifadhi vitunguu kidijitali kupitia mradi wa AOST
25 June 2023, 5:28 pm
Wakulima wa vitunguu kushindwa kunufaika na kilimo cha vitunguu kunatokana na kukosa ujuzi wa kuhifadhi mazao hivyo huwalazimu kuyauza kipindi ambacho mazao mengi yanakua sokoni.
Unapotumia njia ya kidigitali ya uhifadhi wa vitunguu utakusaidia kuwa usalama wa mazao yako na hata kupunguza kwa asilimia kubwa kuharibika kwa vitunguu.
Na Asha Madohola
Imeelezwa kuwa zaidi ya asilimia 30 ya vitunguu hupotea na vilivyosalia hupungukiwa ubora kutokana na wakulima kutumia mabanda yaliyojengwa kienyeji na kuwasababishia kupata hasara muda wa masoko ukifika.
Hayo yalibainishwa katika kata ya Lumuma wilayani Kilosa na mtafiti wa uhifadhi wa zao la vitunguu katika hatua ya uvunaji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Bw Ayubu Eliah ambaye alisema kuwa wamegundua njia bora na ya gharama nafuu ya uhifadhi wa vitunguu kwa kutumia teknolojia iitwayo Airflow Onion Storage Technology ambayo itaruhusu hewa kupita katika eneo la kuhifadhia na kupunguza vitunguu kuoza.
Bw Ayubu alisema kuwa kwa kutumia njia hiyo ya kidigitali ya uhifadhi wa vitunguu utasaidia pia kutunza vitunguu kwa muda mrefu kuanzia miezi mitatu hadi sita na kupunguza mrundikano wa mazao sokoni wakati wa mavuno pamoja na utaongeza ufanisi wa soko ndani na nje ya nchi kwa kuwa vitakuwa vimehifadhiwa katika namna bora hivyo haitapunguza thamani ya vitunguu.
“Kama mkulima akitumia teknolojia hii ya uhifadhi wa vitunguu basi itawezesha vitunguu kupata hewa safi na kupunguza asilimia kubwa ya kuharibika lakini pia mkulima atauza kwa muda ambao ataona unafaa kwa soko kutokana na bei iliyopo” alisema Bw Ayubu
Akizungumza katika ziara ya Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof Palamagamba Kabudi katika kata hiyo kwa niaba ya wanufaika wa mradi huo wa teknolojia ya uhifadhi vitunguu baada ya kuvuna Bw Briton Senyagwa alishukuru kwa jitihada za Mbunge huyo kuwaletea watafiti ambao wamefundisha namna bora ya utunzaji wa vitunguu na wameomba kupatiwa soko ili kupunguza unyonyaji na walanguzi kwa kuwafuata mashambani.
Naye diwani wa kata ya Lumuma Mhe Bakina Zakaria alisema wamenufaika na mafunzo waliyopewa ambayo yatawasaidia kutunza vitunguu kwa njia bora ili kusubiri kuuza kwa bei nzuri ambapo awali walikua wakijenga mabanda mafupi ambayo yalisababisha vitunguu vingi kuoza na kupoteza ubora wake.
Kwa upande wake Mbunge Prof Palamagamba Kabudi aliwashukuru watafiti hao kwa kumaliza muda wao na kuwapatia mafunzo wakulima namna bora ya utunzaji wa vitunguu vyekundu ambavyo ndio vina soko kubwa duniani kote na kwamba dhamira yake ni kuhakikisha kata za Malolo Kidete na Lumuma kunakua ndio kitovu cha upatikanaji wa vitunguu.