Wakulima washauriwa kutumia mbolea ya mboji kuzalisha mazao yenye ubora
21 June 2023, 4:10 pm
Katika kuhakikisha thamani ya mazao yanayolimwa wilayani Kilosa inaongezeka sokoni ni wajibu kwa wakulima kutumia mbolea za mboji na kuzalisha mazao yasiyo na kemikali za mbolea ya viwandani ambayo mazao hayo yanauzwa kwa gharama kubwa katika masoko ya nje.
“Acheni kutumia mbolea za viwandani kwenye ardhi ambazo bado hazijachoka wenzetu huko duniani hawatumii mazao yaliyozalishwa kwa mbolea za kemikali na wapo tayari kununua mara mia zaidi ya bei iliyopo sokoni kwa mazao ambayo hayakuwekwa mbolea za viwandani“.
Na Asha Madohola
Wakulima wa kijiji cha Mnozi kilichopo kata ya Lumuma wilayani Kilosa wameshauriwa kuacha kutumia mbolea za viwandani mashambani kama ardhi bado ina rutuba halisia ambayo inasaidia kuzalisha mazao bora yasiyo na kemikali ambayo yatauzika kwa gharama kubwa.
Hayo yameelezwa kijijini hapo katika mkutano wa hadhara wa mbunge wa jimbo la Kilosa Prof. Palamagamba Kabudi wakati akijibu kero za wananchi ikiwemo ya ukosekanaji wa mbolea za ruzuku ambapo aliwapongeza wakulima kwa kununua kwa wingi mbolea za ruzuku zilizofika katani hapo tani 157.4 huku akishauri kuacha kutumia mbolea kama ardhi haijachoka.
“Tumieni mbolea za viwandani kama ardhi imechoka kama bado haijachoka tumieni mboji ambayo itasaidia mazao yasiwe na kemikali ya madawa ya mbolea na yatauzika duniani kote kwa bei ya juu ila msitumie mbolea za viwandani kama fasheni ili mazao yetu yakauzike nje ya nchi”.
Akijibu changamoto ya barabara kijijini hapo ya kutoka Msowero hadi Mnozi Prof. Kabudi alisema kuwa anatambua umuhimu wa barabara hiyo kwa kuwa wananchi wa Mnozi ni wakulima wa maharage na wanunuzi wanaenda kuyanunua kijijini humo licha ya barabara mbaya iliyopo na halmashauri inapata mapato kupitia ushuru na wananchi wamejitolea kutengeneza barabara hiyo kwa mikono ataiombea fedha serikalini kwa ajili ya matengenezo ya kudumu.
Hata hivyo Prof. Kabudi alizungumzia kutokuwepo kwa zahanati katika kijiji hicho ambapo aliwataka wananchi hao watafute eneo na waanze ujenzi na kwamba atawapatia fedha za mfuko wa jimbo na jengo litakapofikia hatua ya kenchi atatafuta fedha kwa ajili ya mabati.
Katika hatua nyingine Prof. Palamagamba Kabudi aliwataka wananchi hao kupanda miti ya matunda jamii ya maparachichi ili kuondokana na mabadiliko ya tabia nchi iliyoikumba dunia hivyo wanao wajibu wa kuyatunza mazingira kwa kushirikiana ambao utawanusuru na janga la ukame.
Awali wakizungumza na wananchi wa kijiji hicho cha Mnozi akiwemo Monica Safi na Severini Mwaswenya walisema katika kijiji chao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazochangia kuwakwamisha katika masuala ya maendeleo ikiwemo ya ukosekanaji wa zahanati ambapo inawalazimu kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya na ubovu wa barabara.