Mradi wa BOOST Kilosa kujenga shule mpya Mtumbatu
30 May 2023, 10:14 am
Serikali imedhamiria kuondoa adha za sekta ya elimu nchini kwa kuwaletea mradi wa Boost ambao umeanzishwa kwa makusudio ya uboreshaji wa miundombinu kwa madarasa ya awali na msingi, kuimarisha mapito ya wanafunzi wa awali na msingi kwa kuweka mpango wa shule salama na kuimarisha na kuboresha mpango wa mafunzo endelevu kazini kwa walimu wa madarasa ya awali na msingi mashuleni.
“Tumekuwa wa kwanza katika kutekeleza mradi huu wa Boost hivyo ni wajibu wetu kuungana kushirikiana ili kuikamilisha tusipofanya hivyo tutawwanyima wengine kutopatiwa fedha za miradi na hapa tukapunguziwa fedha hivyo lazima tuoneshe kwamba tuna dhamira ya dhati na mradi huu”.
Na Asha Madohola
Wananchi wa kata ya Mtumbatu iliyopo wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wametakiwa kuupokea na kutekeleza mradi wa Boost kwa kushiriki ipasavyo katika utoaji wa nguvu kazi kwenye ujenzi wa shule mpya ya msingi ambao utapunguza kero ya wanafunzi kusomea nje.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara Mbunge wa jimbo la Kilosa Prof Palamagamba Kabudi aliishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijenga sekta ya elimu nchini ambayo ilikua ikikabiliana na changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati.
Prof Kabudi alisema kuwa kata ya Mtumbatu imekua ya kwanza kupelekewa mradi wa Boost ambao upo mahusus kwa kuboresha na kuimarisha elimu ya awali na msingi Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuboresha miundombinu ya madarasa na ili kukamilika inahitaji ushiriki wa nguvu kazi za wananchi.
“Katika mkoa wa Morogoro wenye halmashauri tisa tumepewa shule 17 na halmashauri ya Kilosa tumepewa shule nne katika jimbo la Kilosa shule 3 na Mikumi shule moja kwahiyo ndugu zangu wananchi jambo la msingi ni kujitolea na uwezo huo tunao” alisema Prof Kabudi.
Akizungumza Afsa Elimu Msingi Wilaya ya Kilosa Bi Zakia Fandey alisema wananchi kata hiyo wanapaswa kujivunia kuwa waanzilishi wa utekelezaji wa mradi huo ambao ukikamilika utaondoa adha ya mrundikano wa wanafunzi katika darasa moja na kwa kuwa mradi huo ni shirikishi wanatakiwa kujumuika kwa pamoja ili kuleta matokeo chanya kwa haraka.
Kwa upande wa mratibu wa mradi wa Boost wilayani Kilosa Nelson Kiliba alisema mradi huo umedhamiria uboreshaji wa miundombinu, shule salama, kuwaongezea walimu ujuzi na kwa mwaka huu fedha umeanza kutekelezwa na mradi huo kwa awamu ya kwanza umeanzwa kutekelezwa kata ya Mtumbatu kwa ujenzi wa shule mpya yenye vyumba vya madarasa saba.
Naye Eng Eliud Maeda mshauri wa mradi wa Boost alisema wamejipanga vizuri kutoa utaalamu kwa ushauri kwenye kamati ya ujenzi wa majengo ambapo wanatarajia kuwa na majengo yakinifu ambayo yatatumika kwa muda mrefu.