Wazazi na walezi shirikianeni na walimu kuwapatia malezi bora watoto
19 May 2023, 3:19 pm
Kushamiri kwa vitendo viovu vya ubakaji na ulawiti wa watoto wa kiume na wa kike vinavyofanywa na wananchi wasiokuwa na maadili mema serikali imedhamiria kuwekeza nguvu zaidi katika kukomesha vitendo hivyo vinavyotokea hususan kuanzia ngazi ya familia, shuleni na mitaani.
“Matatizo ya mmomonyoko wa maadili kwa watoto kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na wazazi na walezi kwa kuwapa uhuru uliopotiliza na kujisahau wao ndio wanajukumu la kumlea mtoto sio mtoto kumlea mzazi”.
Na Asha Madohola
Kutokana na kuwepo kwa wimbi la matukio ya ulawiti na usagaji nchini wazazi na walezi wilayani Kilosa wameaswa kushirikiana kwa pamoja na walimu ili kuwapa watoto malezi bora kwa kuwapatia huduma muhimu kama elimu na ulinzi.
Akizungumza katika wiki ya maadhimisho ya siku ya Familia duniani Mwalimu Scolastica Pius Mkwama ambaye ni Mwalimu wa Malezi katika shule ya Sekondari Dendego iliyopo wilayani hapa alisema kuwa kwa kushirikiana na wazazi katika malezi kutawanusuru watoto katika mnyororo wa mmomonyoko wa maadili.
“Kila familia ina changamoto zake hivyo kama walimu tunapokutana na wazazi katika vikao tunajitahidi kuwashauri watoe malezi bora kwa watoto wawapo majumbani mwao ili kuwanusuru kujiingiza katika masuala ya ushoga” alisema Madam Scolastica.
Afsa ustawi wa jamii kata ya Mbumi Bi Zakia Ally Matuila alisema katika maadhimisho ya familia wameamua kutembelea katika shule za msingi ma sekondari ili kutoa elimu ya kujikinga na matukio ya kikatili yanayowakumba kutokana na mmomonyoko wa maadili uliopo.
Naye Elistone Daniel Elibahati Afsa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya wilaya ya Kilosa alisema dhamira ya kutembelea katika shule ni kutoa elimu ya kupinga ukatili na kuimarisha upendo katika familia kupitia elimu hiyo itawasaidia kuibua matukio na kuyaripoti sehemu husika.
Kwa upande wake Afsa Ustawi wa jamii wilayani hapa Bi Leah Mayage aliwataka wanafunzi kuacha kushiriki katika mapenzi ya jinsia moja kutokana kufanya hivyo ni kosa kisheria na wanapaswa kutoa taarifa wanapofanyiwa ama kuoona mtoto anafanyiwa ili sheria ziweze kuchukuliwa watakaobainika kufanya hivyo.
Siku ya Kimataifa ya Familia huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Mei ili kukuza ufahamu wa umuhimu wa familia katika maisha kwenye ulinzi na usalama wa watu wake, malezi, maadili na upendo na kwa mwaka huu yapo chini ya kaulimbiu isemayo Imarisha Maadili na Upendo kwa Familia Imara.