Watoto waaswa kutoa taarifa wakifanyiwa ukatili wa ubakaji
28 April 2023, 1:42 pm
Ili kukomesha vitendo vya kikatili vya ubakaji viongozi na wananchi wanatakiwa kuungana kwa pamoja ili kupinga vitendo hivyo kwa kuwa vinachangia kudhorotesha ndoto za watoto na wengine kupata mimba za utotoni.
Watoto kwa bahati mbaya mkifanyiwa ukatili huo toeni taarifa kwa watu wenu wa karibu kama wazazi, walezi na walimu ili kuwanusuru na matukio hayo ya ubakaji usifiche wala usiogope eleweni viongozi wenu tunakereka na matukio haya.
Na Asha Madohola
Imeelezwa kuwa vitendo vingi vya ubakaji kwa watoto vimekuwa vikitekelezwa na ndugu wa karibu ndani ya familia hivyo serikali inaongeza mapambano ya kukabiliana na vitendo hivyo vya ukatili nchini.
Hayo yalielezwa na Ndg Omary Ahmed Abdallah ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Kilosa katika miaka 59 ya maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kufanyika shule ya msingi Magubike wilayani Kilosa na kusema suala la ubakaji limekithiri nchini na kuwataka watoto kutowafuata watu wasiowajua.
Ndg Omary alisema matendo hayo ya ubakaji yanafanywa na ndugu ambapo mtoto anakua haelewi kitendo anachofanyiwa kuwa ni ukatili, hivyo amewataka watoto kutoa taarifa kwa watu wao wa karibu ama shuleni kwa walimu.
“Kuna matatizo yametokea kwenye jamii yetu ubakaji umekua ukiongeza kila siku naamini kwa jinsi mlivyo hakuna mtoto mwenye idhaa wa kufanya vitendo vichafu kataeni kushikwa na watu msiowajua” alisema Ndg Omary.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo alisema kuwa katika kuadhimisha siku ya Muungano waliamua kuunga jitihada za kuunga mkono za utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti na amewaagiza viongozi wa kata ya Magubike kuongeza kasi ya upandaji miti.