Kilosa yaja na falsafa isemayo Uongozi wa pamoja kwa maendeleo ya haraka
26 April 2023, 7:31 pm
Wahitimu 256 wa chuo cha ualimu Ilonga watakiwa kwenda kuleta maendeleo yenye tija kwenye sekta ya elimu kwa kutumia ujuzi na maarifa waliyopatiwa kipindi chote ambacho walikua chuoni hapo.
“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan imeweza kuendeleza elimu bila ya malipo kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne na kuongeza hadi kidato cha sita”.
Na Asha Madohola
Ili kufikia azma ya maendeleo endelevu wilayani kilosa Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe Shaka Hamdu Shaka ameahidi kufanya kazi kwa kushirikiana na kutumia falsafa ya Uongozi wa pamoja kwa maendeleo ya haraka ili kuharakisha tija ya kimaendeleo ikiwemo ya kiuchumi.
Aliyasema hayo katika mahafali ya kuhitimu kwa wanafunzi 256 wa Chuo Cha Uwalimu Ilonga kilichopo wilayani Kilosa, nakuiomba jamii kuiunga mkono serikali yao ili kuyafikia malengo madhubuti waliyojiwekea.
Alisema kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanyakazi kubwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu kwa kuendeleza elimu bila ya malipo kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita jambo ambalo linawasaidia watanzania wa hali ya chini kupata elimu bure.
Aidha katika sekta hiyo ya elimu alisema Mhe Dokta Samia Suluhu Hassan amejenga vyuo vya ufundi stadi veta 25 kwa mwaka wa fedha 2021-2022 ili kuongeza ujuzi kwa vijana huku kwa mwaka wa fedha 2022- 2023 vitajengwa vyuo hivyo 63.
Alisema serikali imedhamiria kuleta mageuzi kwenye mitaala ya elimu kwa kufanyiwa maboresho ili kuendana na mahitaji ya sayansi na teknolojia jambo ambalo litasaidia elimu kulizalisha wahitimu watakaomudu ushindani katika sekta ya ajira.
Hata hivyo Mhe Shaka Hamdu Shaka alisema serikali imeendelea kufanya ukarabati wa vyuo nchini lakini serikali pia imejenga madarasa kwa shule za msingi hivyo ameungana na wahitimu hao katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa nchi Mhe Dokta Samia Suluhu Hassan.
“Serikali imejenga madarasa zaidi ya elfu ishirini pamoja ambayo yanatumiwa na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari” alisema Mhe Shaka.