Wakulima wa Kilosa wanashauriwa kupanda alizeti
21 April 2023, 10:42 am
Zao la alizeti ni zao ambalo ni la muda mfupi pia linastahimili mvua kidogo hivyo mkulima atanufaika kwenye mazao ambayo atajikwamua kiuchumi kwa haraka tofauti na mazao mengine.
“Mvua zimerudi kwa kipindi kingine ambacho mkulima awali alipanda mazao kama mahindi na mpunga lakini mvua zilikua chache mazao yakakauka hivyo kwa sasa nawashauri kupanda alizeti”.
Na Asha Madohola
Wakulima wilayani Kilosa wameshauriwa kuziitumia vema mvua zilizorudi katika kipindi hiki kwa kupanda mbegu za muda mfupi ambazo zinastamili ukame.
Akizungumza Afisa kilimo wa kata ya Mbigiri Gerald Gabriel Njimbali amesema kipindi hiki cha mvua wakulima wanatakiwa kuachana na kulima zao la mpunga kwa kuwa mvua zitakapokata hautaweza kumea hivyo kwa sasa wanatakiwa kulima zao la alizeti kwa kutumia mbegu za kisasa.
“Mahindi kipindi cha mvua cha kwanza mahindi yalimea vizuri sana lakini ulitokea ukame ambao uliathiri mazao yote na kwa sasa mvua zimerudi hivyo niwashauri wakulima walime mazao ya alizeti ambayo ni ya muda mfupi lakini hata mvua ikikata yanavumilia ukame”.
Bw Njimbali alisema licha ya kuwahamasisha wakulima kulima katika kipindi hiki kwa kutumia mbegu za kisasa lakini bado mpaka hawana mbegu za ruzuku, isipokuwa wanafanya kazi na makampuni ambayo huwaletea na kuwauzia kwa bei nafuu kwa wakulima waliojisajili.
Hata hivyo Afisa kilimo huyo aliishukuru serikali kwa kuwapatia pikipiki ambayo imewarahisishia kuwafikia wakulima wengi na kuwapatia huduma ambayo italeta tija katika kilimo licha ya kukabiliwa na changamoto ya mafuta.