Mashamba ya malisho yaanza majaribio Kilosa
8 April 2023, 10:40 pm
Serikali ikiwa katika kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani Kilosa imeamua kuanzisha majaribio ya mashamba ya malisho ili kunusuru mifugo kuchungiwa kwenye mashamba ya mazao.
“Tabia ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima imekua ni mazoea kwa kuwa wafugaji wamekua wakilipishwa fidia hiyo haikubaliki na ni kosa la jinai lazima wafunguliwe mashtaka”.
Na Asha Madohola
Wilaya ya Kilosa imeanza kutekeleza mpango wa serikali wa kuanzisha mashamba ya majaribio ya malisho ya mifugo yataakayolimwa katika vijiji vya Madoto na Maguha lengo likiwa ni kupunguza changamoto za migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Akiwa katika mkutano wa hadhara katika kata ya Magomeni Mbunge wa Jimbo la Kilosa Mhe Prof Palamagamba Kabudi alisema mashamba hayo ni kati ya mia moja yaliyoidhinishwa na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya mpango huo.
Prof Kabudi alikemea tabia iliyojengeka ya wafugaji ya kutoa fidia kila wanapolisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima akisema inawajengea usugu wa kuendeleza kufanya uhalifu huo.
“Tabia hii ya wafugaji kulisha kwenye mashamba imekua ya mazoea kwa kuwa wamekua wakilipishwa fidia na hakuna mkulima anayelima ili alipwe fidia”alisema Prof Kabudi.