Milioni 400 zajenga shule yenye madarasa 11 Kilosa
6 April 2023, 11:08 am
Ujenzi wa shule ya msingi Tambukareli iliyopo jimbo la Mikumi wilayani Kilosa umetatua changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufika shule kitendo kilichokuwa hatarishi kwa usalama wao pindi wawapo njia ambapo iliwalazimu kuvuka barabara kuu ili kuifuata shule ilipo.
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutujengea shule hii ambao umepunguza mrundikano wa wanafunzi uliokuwepo awali katika shule zilizokuwepo hii itatoa fursa kwa wanafunzi kusoma katika mazingira bora”.
Na Gladys Mapeka
Halmashauri ya wilaya ya Kilosa imeendelea kuneemeka na fedha mbalimbali toka Serikali Kuu katika kuwaletea maendeleo wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu, kwa uwepo wa ujenzi wa shule ya msingi Tambukareli katika kata ya Mikumi.
Akizungumzia ujenzi wa shule ya hiyo ambayo imezinduliwa rasmi hivi karibuni Mkuu wa Divisheni ya Elimu Msingi na Awali Bi. Zakhia Fandey alisema ujenzi wa shule hiyo umetokana na fedha kutoka Serikali Kuu chini ya mradi wa GPE LANES II kwa shilingi milioni 400, ambapo shule ina vyumba vya madarasa 11.
Fandey alisema shule hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu, kuinua ari ya wanafunzi kupenda shule kutokana na uwepo wa mazingira bora ya ujifunzaji.
Akizungumzia faida na umuhimu wa uwepo wa shule hiyo Mratibu wa elimu kata ya Mikumi Yusta Ndelwa amesema kupitia uwepo wa shule hiyo umepunguza mrundikano wa idadi kubwa ya wanafunzi madarasani, lakini pia itaongeza usalama wa wanafunzi waliokuwa wakisoma shule za msingi za Mikumi, Mikumi Mpya na Mikumi Town ambapo awali walikuwa wakivuka barabara lakini kwasasa watakuwa salama zaidi.
“Tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya sita kwa kuitazama Mikumi kwa jicho la tatu, kwani wamefanikiwa kupata madarasa na madawati ya kutosha sambamba na uwepo wa vyoo stahiki ambavyo pia vimezingatia wanafunzi wenye mahitaji maalum” alisema Bi Yusta.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Ibrahim Chembe amesema kupitia fursa hiyo imewajengea wanafunzi na walimu mazingira na ari nzuri ya ufundishaji na ujifunzaji ambapo imeanza na wanafunzi 432 kuanzia elimu ya awali hadi darasa la sita na kwamba matarajio ni kuwa na wanafunzi 700 kwa shule nzima.