Serikali kuwaunga mkono wananachi watakaonzisha miradi ya maendeleo Kilosa
12 March 2023, 9:30 am
Katika kutambua fursa za miradi ya maendeleo wilayani Kilosa serikali imeahaidi kuunga mkono jitihada zitazofanywa na wananchi.
“Serikali imejipanga kuhakikisha inaendeleza miradi ya maendeleo pamoja na kuwalinda wananchi na mali zao”.
Na Asha Mado
Wananchi wametakiwa kutambua jitihada mbalimbali ambazo serikali inazifanya katika kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira mazuri ikiwemo katika kuwaletea miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.
Rai hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh, Hamad Masauni alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mikumi ambapo amesema Serikali imekuwa ikifanya kazi kubwa katika kuendeleza miradi mbalimbali.
“Hii serikali ya awamu ya sita imejipanga kwa dhati kuwahakikishia wananchi usalama wao na mali zao kwa kuendelea kujenga vituo vya polisi na nyumba za polisi katika maeneo mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kiusalama” alisema Mhe Masauni.
Aidha amelitaka jeshi la magereza kuwekeza zaidi katika kuendelea kutumia rasilimali walizonazo katika kuisadia Serikali kutimiza adhma yake ya kuhudumia wananchi kwa kuwa jeshi hilo lina wataalam wakutosha ambao wana uwezo wa kusababisha mabadiliko chanya kwa jamii na Serikali kiujumla.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mhe Dennis Londo ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa fedha nyingi ambazo Jimbo la Mikumi limepokea kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini pia amemuomba waziri huyo kuongeza nguvu katika kuiesema miji ambayo inapaswa kupewa hadhi ya kuwa halmashauri kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa miradi ya kimkakati.
“Ninaomba kufanyika kwa maboresho ya upatikanaji wa kituo kikubwa cha polisi pamoja na vituo vidogo kwa baadhi ya maeneo kwani maeneo mengi ya wilaya ya Kilosa hayana vituo vidogo vya polisi”alisema Mhe Londo
Kwa upande wa viongozi wa jeshi la Magereza Mkuu wa gereza mkoa wa Morogoro ACP Dkt. Wilson Rugamba na Mkuu wa gereza Kilosa ASP Dominick Mshana wamesema jeshi la magereza liko tayari kutekeleza na kupokea mabadiliko chanya yanayoendelea ndani ya Serikali.
“Tunajipanga kuwa na jeshi la kisasa lenye tija kwa ajili ya kuzalisha hususani katika kilimo kwa kutumia rasilimali zilizopo kutokana na ardhi ya kilimo waliyonayo” alisema ACP Dkt Rugamba