Watendaji kata wakabidhiwa pikipiki Kilosa
11 March 2023, 6:05 pm
Katika kurahisisha utendaji kazi wa kuyafikia maeneo yote yaliyopo katika kata serikali imewapatia maafisa watendaji kata pikipiki ambazo zitawasaidia kuwafikisha maeneo ambayo walikua hawayafikii kiurahisi kutokana na umbali uliopo.
Awali viongozi wa kata walikua wanakabiliwa na changamoto ya usafiri kwa kuona hivyo serikali imedhamiria kuwapa pikipiki watendaji ambapo kwa kuanza wamepokea pikipiki kumi kutoka serikali kuu na wamezikabidhi kwa kata kumi.
Na Asha Mado
Uongozi wa Halmshauri ya Wilaya ya Kilosa umeushkuru uongozi wa Awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani chini ya OR-TAMISEMI kwa kuwatazama watendaji wa kata kwa kuwapatia pikipiki 10 ikiwa ni sehemu ya awamu ya kwanza ya ugawaji wa pikipiki hizo kwa watendaji ambazo zitawasaidia katika majukumu yao ya kuwahudumia wananchi hususani katika kuyafikia maeneo yenye changamoto ya kufikika kwa urahisi.
Akizungumzia makabidhiano ya pikipiki hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba amesema Halmashauri ya Kilosa imepokea pikipiki 10 kati ya pikipiki 916 zilizotolewa kwa watendaji wa kata nchi nzima kutoka 0R- TAMISEMI ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha watendaji wa kata kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.
“Kwa kuanza wakati mgao ukiendelea zimegawiwa kata kumi zilizopo pembezoni ambazo zina changamoto usafiri na kwamba mgao huo utakuwa kwa kata zote”alisema Mkurugenzi Mtendaji Mabuba.
Makabidhiano ya pikipiki hizo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa yamefanywa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mh. Shaka H. Shaka yakishuhudiwa na waheshimiwa madiwani , wataalam pamoja na wadau mbalimbali waliohudhuria kikao,cha baraza la madiwani ambapo kata kumi kati ya arobaini zilizopo katika Wilaya ya Kilosa zimepokea pikipiki ikiwemo kata ya Mtumbatu, Mamboya, Mabula, Berega, Vidunda, Ruhembe, Malolo, Kilangali, Lumuma na Lumbuji.