Suluhisho la utoro na kufeli kwa mitihani shule za msingi lapatikana Kilosa
14 February 2023, 12:48 pm
Shule ya Msingi Mazinyungu inatarajia kunufaika na mradi wa kilimo waliouanzisha ambao utawasaidia wanafunzi kupata chakula cha mchana shuleni hapo na kuwapunguzia gharama za uchangiaji wa fedha za chakula suala ambalo litawawezesha wanafunzi kutumia muda mwingi wakiwa shule kwa ajili ya masomo kitendo ambacho kitaongeza wastani wa ufaulu shuleni.
Na Asha Mado
Imeelezwa kuwa ili kupunguza changamoto za utoro na kufeli katika mitihani kwa wanafunzi wa shule za msingi ni kutokana na ukosekanaji wa kula chakula cha mchana shuleni hususani katika kipindi hiki ambacho gharama za vyakula imekua kubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni katika kikao maalumu cha shule ya Msingi Mazinyungu kilichowakutanisha uongozi wa shule, kata pamoja na wazazi na walezi na kujadiliana namna ambavyo wataweza kuwaidia watoto kwa kuwachangia fedha ya chakula.
Mwenyekiti wa Umoja wa Walimu na Wazazi Salehe Kaombwe amesema jumla ya watoto 130 kati ya 1375 ndio wanapata chakula shuleni hapo na kwamba hali hiyo inachangia kwa kuongezeka kwa utoro shule na wanafunzi kuyakosa ama kuchelewa masomo kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta chakula nje ya shule.
Akizungumza mmoja wa wazazi Edna Rwezaura amesema kuwa kwa kuwa ni agizo la serikali hivyo kwa wazazi inatakiwa ni utekelezaji kwa kuangalia namna gani watapata fedha ili kulipia chakula ili watoto wapate chakula shule licha ya hali ya kiuchumi kuwa ngumu kwa wote.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Mwl Gallan Kajika amesema kuwa kutokana na kusuasua kwa wazazi kuwalipia watoto hela ya chakula kutokana na hali ya kimaisha kuwa ngumu wameamua kulima shamba ili liwasaidie kupata chakula cha shule na kuwapunguzia gharama wazazi.
“Wazazi wa Shule ya Msingi Mazinyungu siyo kwamba wanashindwa kuchangia chakula shule ili watoto wapate chakula cha mchana shule isipokuwa kwa kipindi hiki ambacho kuna hali ngumu ya kiuchumi wazazi wameshindwa kuchangia hivyo nikaamua kuushirikisha uongozi wa shule na viongozi wa Umoja wa Walimu na Wazazi kutafuta shamba ili kuondokana na adha hii na kwa sasa tumeshapanda mahindi shamba lenye ukubwa wa hekari kumi” alisema Kajika
Awali akitoa taarifa katika kikao hicho Diwani wa kata ya Kasiki Ramadhani Bon Mpangachuma amesema kuwa suala la utoaji wa chakula ni la lazima kwa shule zote nchini na ni agizo kutoka serikalini kwamba watoto wote kuanzia darasa la awali mpaka darasa la saba wale chakula cha mchana shule hivyo wazazi wanawajibu wa kuchangia chakula.