Radio Jamii Kilosa

Hatimaye migogoro ya mashamba yatatuliwa Kilosa

4 February 2023, 10:42 pm

Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe akizungumza na Wananchi wa Kata ya Mvumi Wilayani Kilosa.Picha na Epiphanus Danford

Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuwa, ihakikishe inapima eneo la Shamba ambalo Serikali ilikabidhi Halmashauri hiyo na kuwapatia Wananchi kwa kuwapatia hati ndogo inayoonyesha umiliki halali wa eneo hilo.

Na Epiphanus Danford

Waziri huyo wa Kilimo ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuwakabidhi mashamba Wananchi wa Kata ya Mvumi Wilayani humo,mara baada ya kufika katika kata hiyo na kuona Wananchi wakilalamikia mashamba hayo.

Waziri Bashe ameyasema hayo mapema hii leo February 4,2023 alipokutana na Wananchi wa Kata ya Mvumi Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa,Ikiwa ni ziara yake ya siku moja katika Halmashauri hiyo mara baada ya kutolewa agizo la Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Taifa Ndugu,Daniel Chongolo kumtaka Waziri wa Kilimo afike katika Halmashauri hiyo ili aweze kutatua changamoto za Wananchi wa Kata hiyo ya Mvumi kuhusiana na Mashamba yaliyofutwa na Serikali na kukabidhiwa kwa Halmashauri.

”Serikali imefuta Mashamba ili iweze kuwasaidia Wananchi kuwaondoa watanzania hawa kuwa manamba kwenye ardhi yao na maelekezo ya Mhe.Rais ni kwamba Halmashauri inatakiwa ilipime lile eneo lote iwe na hati kubwa moja na hati isome Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Wizara ya Kilimo.Alisema Waziri Bashe.

Waziri wa Kilimo akitoa ufafanuzi wa mashamba hayo kwa Wananchi wa kata ya Mvumi Wilayani Kilosa.

Sambamba na hayo,Waziri Bashe amepiga marufuku kukodishwa kwa Mashamba hayo na madala yake wapewe Wananchi wa eneo husika,na kuwaambia viongozi wa ngazi ya Mkoa na Halmashauri kuacha mara moja kuwakodishia wananchi mashamba yaliyofutwa na Serikali na badala yake wakabidhiwe wananchi.

 

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akitoa maagizo ya Serikali kwa viongozi wa mkoa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.

Waziri Bashe amemaliza ziara yake kwa kuitaka Halmashauri kuwakabidhi Wananchi maeneo yao ili kusudi waondokane na suala la umaskini kwani Mwananchi asipomoliki ardhi ndiyo umaskini mkubwa.Alisema Waziri Bashe.

Nao baadhi ya Wananchi wameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa uamuzi huo uliotolewa na Waziri Bashe kwa kuitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Iwagawie Wananchi hao Mashamba ili kusudi waweze kulima kwani yatawasaidia kupunguza umaskini.