Radio Jamii Kilosa

Waziri Ndaki awataka wafugaji kubadilika.

30 January 2023, 9:32 am

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mashimba Ndaki (Mb)amewataka wafugaji kubadilika kwa kuacha mfumo wa ufugaji wa mazoea kwa kutegemea ardhi ya Jumuiya na badala yake wawe na eneo la kufugia Mifugo Yao eneo ambalo atatumia liwe linatambulika kisheria.

Waziri Ndaki ameyasema hayo 26 Jan 2023 katika Kijiji Cha  Mbwade akiwa katika ziara yake ya kikazi Wilani Kilosa Mkoani Morogoro ambapo Katika ziara hiyo ameambatana na Viongozi mbalimbali kutoka Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa akiwembo Mbunge wa Jimbo la Kilosa,Mwenyekiti Wa Halmashauri na wengineo.

Aidha Waziri Ndaki amewataka wafugaji kuacha Mara moja tabia ya kupeleka Mifugo kupata malisho Katika Mahamba ya wakulima kwani kufanya hivyo inaweza kupelekea migogoro ya wakulima na wafugaji isiyoisha.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh.Mashimba Ndaki akizungumza na Wafugaji Wilaya ya Kilosa
Waziri wa Mifugo na Uvuvi akiwasihi wafugaji kuhusu sheria ya kupeleka Mifugo katika Shamba la Mtu.

Sambamba na hayo pia amewataka Wafugaji na wakulima kushirikiana Katika Shughuli zao na Kuacha kuvutana kwani kwa kufanya hivyo itapelekea kurudisha maendeleo nyuma.

Kwa Upande wake Dkt Yuda Mgeni Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi amemshukuru Mhe Waziri kwa kuweza kufika wilayani Kilosa ambapo amesema wafugaji wanatakiwa kufuga kibiashara na kufuga mifugo yenye tija kwa ajili ya soko la ndani na nje ambalo litaendana na mabadiliko ya Tabianchi.

Dkt Yuda amesema kwa sasa maeneo ya malisho yamezidi kupungua hivyo wajitahidi kuwa na maeneo ambayo yatasaidia kwa ajili ya malisho pia amewaomba wafugaji kuachana na migogoro na kujikita katika ufugaji wenye tija.