Tanesco kumaliza tatizo la kukatika umeme Kilosa- Meneja Tanesco
26 January 2021, 11:37 am
Shirika la Umeme Tanzania Tanesco wilayani Kilosa limejipanga kikamilifu kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara katika baadhi ya maeneo kunakosababishwa na nguzo chakavu zilizooza ama kuanguka.
Akizungumza Januari 26 2021 katika kipindi cha Mambo Mseto kinachorushwa na Radio Jamii Kilosa Meneja wa Tanesco Wilaya Kilosa Daniel Makala Kingu amesema kuwa miundombinu ya umeme ni mibovu katika baadhi ya maeneo hususani Mtaa wa Mtendeni.
Kingu amesema kuwa Tanesco Kilosa imejipanga kuondoa nguzo zote zilizooza katika maeneo ya miji na vijijini kwenye laini zinazosafirisha umeme kwenda majumbani kwani tayari taratibu za kupata nguzo mpya zimeshafanyika.
Hata hivyo amewaomba wananchi kutoa taarifa mapema Tanesco pindi wanapoona hitilafu ya umeme imetokea katika maeneo yao ili hatua za haraka zichukuliwe kabla madhara makubwa kutokea.
Sambamba na hayo pia amewataka wananchi kuwa na vifaa vya kuzuia umeme usilete hitilafu katika majengo ikiwemo waya wa Ethi wa kuzuia radi ili pindi unapokatika na kurudi usilete madhara ndani ya nyumba .