FM Manyara

DC Kaganda aonya watoto chini ya miaka 5 kutozwa gharama za matibabu

12 January 2026, 2:20 pm

Picha ya Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Mtatifikolo Kaganda akiwasalimia baadhi ya wagonjwa

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Mji Babati kufuatia malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kutozwa fedha kwa matibabu ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano, kinyume na maelekezo ya Serikali.

Na Mzidalfa Zaid

Katika ziara hiyo, Kaganda amezungumza na baadhi ya wazazi waliothibitisha kuwa wamekuwa wakitozwa fedha licha ya watoto wao kuwa na sifa ya kutibiwa bure ambapo Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya alitoa onyo kali kwa uongozi wa hospitali hiyo kuacha mara moja tabia hiyo na kuzingatia maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwamba watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na wazee wasiojiweza wanatakiwa kupatiwa matibabu bure, kwani huduma hizo zimeshalipiwa na Serikali.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Mtatifikolo Kaganda

Amewataka wazazi na walezi kutoa taarifa mara moja iwapo watakumbana na changamoto kama hiyo. Vilevile, amewahimiza wazee wenye changamoto za kupata huduma kufikishwa kwa Watendaji wa Kata na Vijiji ili taarifa zao ziwasilishwe kwa Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kupewa huduma stahiki.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko kwa kuchemsha maji kabla ya matumizi, kama njia ya kujikinga na maradhi hatarishi.