Jumuiya ya Wazazi wilayani Kilosa waishauri serikali kuikarabati shule iliyoingia mafuriko miaka 14 iliyopita
29 April 2023, 11:07 am
Ni zaidi ya miaka kumi shule ya msingi Madaraka imehamishwa kutokana na mafuriko yaliyoingia shuleni hapo na kupelekea wanafunzi kuhamishwa Jumuiya ya wazazi wameishauri serikali kuikarabati shule hiyo.
“Majengo tumeyaona na tatizo kubwa lililofanya shule hiyo kuhamishwa ilikuwa ni mafuriko kwa sasa ni zaidi ya miaka kumi na mafuriko hakuna ni vema tuwarudishie shule yao maana shule yao ipo”.
Na Asha Madohola
Serikali imeshauriwa kuifanyia ukarabati shule ya msingi Madaraka iliyopo kata ya Mbumi wilayani Kilosa ambayo iliingiwa na mafuriko zaidi ya miaka kumi iliyopita ili kuwapunguzia umbali mrefu wanafunzi wanaotembea kufuata shule ilipohamishiwa.
Hayo yamejiri katika ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilayani Kilosa Mhe Omary Ahmed Abdallah aliyefika katika majengo ya shule hiyo na kujionea hali halisi iliyopo na kubaini kuwa bado majengo hayo yana uimara.
Mhe Omary alisema kutokana na adha wanazozipata watoto ya kutembea umbali mrefu huku wakikutana na changamoto mbalimbali njiani ikiwemo kufanyiwa vitendo vya kikatili serikali inatakiwa kuirudisha shule hiyo kwa haraka ili kuwaepusha watoto na madhira hayo.
“Kujenga madarasa mapya ni sawa ila ni gharama kubwa lakini kufanya ukarabati ni bora zaidi kwa kuwa serikali imeboresha mifereji hivyo maji hayataingia tena katika shule hiyo” alisema Mhe Omary.
Awali akitoa maelezo ya shule hiyo diwani wa kata ya Mbumi Mhe Shaban Malingo alisema kuwa kuhamishwa kwa shule hiyo imekua changamoto kwa wanafunzi, na shule hiyo ikikarabatiwa itawasaidia na watoto kutoka kata jirani.