Serikali yasikia kilio cha shule ya mbao yatoa zaidi ya shilingi 400 kujenga shule ya kisasa Kilosa
7 April 2023, 1:07 pm
Adha wanayoipata kwa sasa wanafunzi wa shule ya msingi Mambegwa ni kukaa chini pamoja na kusomea kwenye majengo ya muda yaliyojengwa na wananchi baada ya majengo ya kudumu ya shule hiyo kusombwa na maji.
“Ni zaidi ya mara mbili shule hii kusombwa na maji hali inayopelekea kukatisha masomo kwa wanafunzi kwa kushirikiana wazazi tuliamua kujenga shule ya muda ya mabanzi ili watoto wetu wasome wakati serikali ikifanyia kazi ombi let la kujengewa shule”.
Na Asha Madohola
Hatimaye kijiji cha Mambegwa kilichopo kata ya Msowero wilayani Kilosa kimepatiwa zaidi ya shilingi milioni mia nne iliyotolewa na serikali kwa ajili wa ujenzi wa shule ya kudumu ambayo itakua mbadala ya iliyopo kwa sasa iliyojengwa kwa mabanzi na mabati.
Wakizungumza wananchi wa kijijini hapo Antonia Nyambuya amesema kuwa mafuriko yaliyotokea mwaka jana ulipelekea majengo ya shule kusombwa na maji na wakaamua kujenga majengo ya muda ambayo sio rafiki kwa watoto kusomea hapo.
“Tumekuwa wahanga wa mafuriko kwa zaidi ya mara mbili na kupelekea shule kusombwa na maji hivyo kwa kushirikiana na serikali ya kijiji tuliamua kujenga majengo ya muda ili watoto waendelee kupatiwa elimu lakini mazingira hayana usalama” alisema Bi Antonia.
Naye Laurent Teuke ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt Samia kwa kukiona kijiji chao kwa jicho la tatu na kuwapatia kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo Masatu Mbotho amesema hali ya ufundishaji imekua na changamoto kutokana na shule ya muda imejengwa sehemu tofauti ilipo shule mama.
Mbunge wa Jimbo la Kilosa Mhe Palamagamba Kabudi aliyefika katika kijijini hapo kuzungumza na wananchi amesema anamshukuru Rais Dkt Samia kwa kusikia kilio chake cha kuomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo na hatimaye ametekeleza kwa vitendo kwa kuwapatia fedha zaidi ya milioni mia nne ambapo anatarajia itajengwa shule nzuri na ya kisasa.