Wananchi walia na baa la njaa Kilosa
6 April 2023, 4:16 pm
Wananchi wa kitongoji cha Karadasi kilichopo kijiji cha Mambegwa kata ya Msowero wilayani Kilosa wameiomba serikali kuwaletea chakula cha msaada ambacho watakinunua kwa gharama nafuu.
“Hali ya ukame imekua tishio la baa la njaa kijijini hapa mazao yote yamekauka na mahindi mpaka sasa tunanunua sado shilingi elfu nane tunaiomba serikali itusaidie wananchi wake tunakufa na njaa” .
Na Asha Mado
Kutokana na hali ya ukame iliyopita katika kipindi cha msimu wa kilimo na kupelekea mazao ya wakulima kukauka kabla ya kufikia hatua ya uvunaji hali iliyopelekea kuiomba serikali kupeleka msaada wa chakula katika kijiji cha Mambegwa Kitongoji cha Karadasi ili kuwaepusha na baa la njaa ambalo linaonekana kuingia kwa katika kipindi kifupi kijacho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wakiwa katika mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Kilosa Paramagamba Aidan Kabudi aliyefika kusikiliza kero na kuzitatua wamesema hali ya kiuchumi katika kijiji hicho imekua ngumu kutokana na kushindwa kunufaika na kilimo walicholima kukauka na jua.
Mmoja wa wananchi hao Sara Surua Majura licha ya kukabiliwa na changamoto ya ukame ambalo limewaathiri kiuchumi pia wanakabiliwa na wafugaji kuingiza mifugo kwenye mazao na kusababisha kuzuka kwa migogoro ya wakulima na wafugaji
Naye Charles Kahila Hanu balozi wa Karadasi amesema kuwa njaa imekua tishio katika eneo lao ameiomba serikali kuwapatia chakula cha msaada na mbegu za muda muda mfupi ili mvua zilizoanza kunyesha wapande mazao.
Aloyce Karoli Isutya amesema kuwa awali eneo lao lilikuwa na rutuba ya kutosha na walikua wanapata mazao mengi lakini kutokana na ukataji wa miti uliofanywa wa wananchi umepelekea mvua kuwa za kusuasua hivyo amewataka wananchi wenye mashamba kupanda miti na kwamba mifugo imekua chanzo cha kuharibu mashamba.
Awali akizungumza katika mkutano huo Nyansio Gregory katibu wa vijana chama cha Mapinduzi wilaya ya Kilosa alisema hali ya mazao Karadasi ni mbaya kutokana na kuathiriwa na ukame na hivyo amewataka watendaji kuanzia kijiji kuchukua za haraka za kufanya tathmini ili kuwanusuru wanachi hao na baa la njaa.
Kwa upande wake Mbunge huyo Mhe Kabudi amesema kuwa ameshukuru kuona wananchi wamebaini ukame uliopo kwa sasa umesababishwa na uharibifu wa mazingira kwa kufyeka miti ya asili hivyo amewaomba wananchi hao kutunza mazingira ili kurudisha rutuba iliyopotea.