Kikundi cha Kiwasai chafaidika na vifaranga vya samaki 1000.
16 April 2021, 11:19 am
Katika kuhakikisha jamii inaepukana na changamoto ya udumavu, Shirika la Save the Children kupitia mradi wa Lishe endelevu unafadhiliwa(USAID) April 15 umetoa vifaranga vya samaki aina ya Sato elfu moja katika kikundi cha KIWASAI kilichopo Ilonga Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.
Mratibu Mradi wa Lishe endelevu Mkoa wa Morogoro Anania Josia amesema kuwa lengo la kutoa vifaranga hivyo kama kianzio katika Halmashauri ili waweze kuzaliana ili wafugaji wengine waweze kuchukua mbegu hiyo iliyoboreshwa ambapo vifaranga hivyo pamoja na kilo 30 za chakula cha vifaranga vimekabidhiwa kwa kikundi hicho na Mwenyekiti wa Halmashauri wa Wilaya ya Kilosa Mh. Wilfred Sumari.
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Wilfred Sumari baada ya kukabidhi vifaranga hivyo ameushukuru Mradi wa Lishe endelevu kutoa msaada wa vifaranga hivyo na kuongeza kuwa ufugaji wa samaki utasaidia wananchi kupata chakula bora na kupunguza tatizo la udumavu Wilayani Kilosa.
Kwa upande wao wanakikundi wa KIWASAI wameushukuru Mradi wa Lishe endelevu kwa kuweza kuwapatia msaada huo na kuahidi kugawa mbegu kwa watu wengine ambao wanahitaji kujihusisha na Ufugaji wa samaki.