Radio Jamii Kilosa

DC Shaka: Hamasisheni wananchi ushiriki uchaguzi serikali za mitaa

31 August 2024, 8:17 am

Mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe Shaka Hamdu Shaka akizungumza katika baraza la madiwani. Picha na Kitengo cha mawasiliano serikalini.

“Ustawi wa mwananchi wilayani Kilosa unategemea busara za Baraza hili, kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa manufaa ya wana Kilosa na Taifa kwa ujumla na mkatumie mikutano yenu ya hadhara kuwahamasisha wananchi kujitokeza na kutumia haki yao ya Kidemokrasia ya kuchagua Viongozi wa Vijiji,Vitongoji na Mitaa” alisema Mhe Shaka

Na Asha Madohola

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe Shaka Hamdu Shaka amewataka Viongozi wa ngazi zote kuhamasisha na kuhabarisha Wananchi juu ya uwepo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotajariwa kufanyika Novemba mwaka huu ili waweze kujitokeza kwa wingi katika kushiriki kuanzia kujiandikisha mpaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Mhe. Shaka aliyasema hayo 29 Agosti, 2024 wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani wa kupitia na kujadili taarifa mbalimbali za utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kwa kipindi cha robo ya nne (April-Juni) kilichofanyika katika Ukumbi wa FDC Ilonga.

Waheshimiwa Madiwani wakiwa kwenye Mkutano wa baraza la madiwani

Mhe Shaka aliwataka viongozi hao kuhamasisha wanawake na watu wenye ulemavu watakaokuwa na sifa za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika vijiji na vitongoji kuchukua fomu na kuomba nafasi za uongozi.

Aidha alisema kuwa katika uchaguzi huo hali ya Usalama na Amani wilayani Kilosa itazingatiwa ili uwe Dira na Kioo cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 wa kuchagua Rais,Wabunge Pamoja na Madiwani.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Mhe Wilfred Sumari

Hata hivyo alimshukuru Mhe. Mwenyekiti wa Halmashauri na Baraza lake la Waheshimiwa Madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Timu ya Menejimenti kwa ushirikiano unaoendelea kuoneshwa katika mambo mbalimbali ya Maendeleo na kwamba matumaini yake kuwa katika zoezi zima la uchaguzi umoja na mshikamano huo utaimarika maradufu.