Prof. Kabudi afuturisha mamia ya wakazi Rudewa
9 April 2024, 1:09 pm
Zimesalia siku chache ili kuisha kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambapo waislam duniani kote wamekuwa wakitimiza moja ya nguzo muhimu ya dini kwa kufunga na kufanya ibada na matendo mema huku wakidumisha amani, upendo na ushirikiano baina yao.
Na Asha Madohola
Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof. Palamagamba Kabudi amewataka waumini wa dini ya Kiislam na dini zingine katika madhehebu tofauti wilayani Kilosa kulinda misingi ya amani iliyoasisiwa na waasisi wa taifa la Tanzania kwa kuwataka wananchi kuendelea kufanya matendo mema kama ambavyo wamekuwa wakiyatenda kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Akizungumza na mamia ya waumini wa dini ya Kiislam wilayani Kilosa walioungana pamoja kushiriki katika iftar iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof. Palamagamba Kabudi katika msikiti wa Rudewa na kuhudhuriwa na viongozi wa dini mbalimbali akiwemo Sheikh Mkuu wa wilaya, kiongozi wa dini mbalimbali, alisema misingi ya amani ikiendelea kuasisiwa vyema itajenga jamii bora yenye upendo na kulitumikia taifa kwa uzalendo.
Aidha Prof. Kabudi aliongeza kwa kusema kuwataka waumini wa dini ya kiislamu kuendelea kuyaishi maisha waliokuwa wakiishi katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani uliowajenga waumini hao kiimani, kuwa na hofu ya Mungu,kufanya ibada na kuyaacha matendo maovu.
“Kipindi hiki tunatakiwa kuendeleza mioyo ya upendo na ushirikiano hata mwezi Mtukufu wa Ramadhani utakapoisha na muhimu ni kuheshimiana kwa dini zote ili kuleta amani katika Taifa letu na ndio tutawajenga vijana kiimani na kuwa wazalendo” alisema Prof Kabudi.
Hata hivyo alitumia jukwaa hilo kuwaeleza wananchi juu ya neema kubwa na baraka za Mwenyezi Mungu kwa kuwanusuru wakazi wa Rudewa na janga la mafuriko yaliyotokea wilayani hapo na kuwasihi waendelee kushika imani za dini huku aliwataka kuendelea kuliombea amani Taifa pamoja na kumuombea afya njema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Awali akimkaribisha Mbunge huyo, Sheikh Mkuu wa Wilaya Kilosa, Sheikh Nassoro Milambo alipongeza jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi wa Kilosa maendeleo makubwa ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya Barabara, Shule mpya za Sekondari pamoja uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano.
Sheikh Milambo alisema Maendeleo hayo makubwa kamwe hayajawahi kutokea na kukiri kuwa yanatokana na kumpata Mbunge mwenye kufanya kazi kwa weledi na upendo kwa wananchi wake kwa kuendelea kusimamia shughuli za kimaendeleo wilayani hapo.
Aidha katika Iftari hiyo Waumini wa dini ya Kiislamu wakiongozwa na Shekh Mkuu wa Wilaya walifanya dua maalumu kwa kuliombea Taifa na kumuombea Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliongoza Taifa vyema pamoja na kumtakia heri Mbunge wao kusimamia vyema miradi inayotekelezwa jimboni humo itakayosaidia kuchagiza uchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.