Prof. Kabudi akagua miradi ya shule, ahimiza wazazi kuwasomesha watoto
18 March 2024, 1:50 pm
Katika kuhakikisha elimu inawafikia watoto wote nchini serikali imewekeza kuhakikisha shule za awali, msingi na sekondari zinakuwepo za kutosha hususan vijijini ambapo ilikuwa inawalazimu watoto kutembea umbali mrefu kwenda shule.
Na Asha Rashid Madohola
Mbunge wa jimbo la Kilosa Prof. Palamagamba Kabudi amewataka wazazi katika kijiji cha Kitange mbili kata ya Mtumbatu wilaya kilosa mkoani Morogoro kutozuia watoto kwenda shule kutokana na idadi ndogo ya watoto wa waliotakiwa kuripoti kuanza kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Kitange.
Prof. Kabudi ameyasema hayo katika ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya shule ambapo amefika katika shule hiyo ambayo ujenzi wa vyumba vya madarasa unaendelea huku akiwataka wananchi hao kuhakikisha watoto wanakwenda shule ili kuunga mkono juhudi za serikali inayotoa fedha kwaajili ya ujenzi wa shule katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Shule hiyo mpya ya sekondari Kitange ujenzi wake ulianza mwaka 2022 kwa nguvu kazi ya wananchi baada ya wanafunzi kutembea umbali mrefu wa takribani zaidi ya kilometa 10 kufuata huduma ya shule ambapo hadi sasa ni madarasa mawili pekee ndio yaliyokamilika kwa hatua ya awali kwaajili ya wanafunzi kuanza masomo kwa kidato cha kwanza kwa mwaka huu wa 2024.
Akitoa taarifa ya mradi huo mkuu wa shule hiyo bi.Cecilia Chipeta amesema Licha ya wananchi kuanza kwa kujitolea nguvu kazi wadau na serikali haikuwaacha nyuma na sasa ujenzi wa vyumba vingine vya madarasa unaendelea huku aibainisha kuwa hadi sasa wanafunzi 84 pekee ndio walioripoti kati ya wanafunzi 198 wa kidato cha kwanza waliopangiwa katika shule hiyo.
Naye katibu wa wazazi cha chama cha mapinduzi(CCM) wilaya ya Kilosa Selina shayo alisikitishwa na taarifa ya watoto kutokuhudhuria shule na kuwahimiza wazazi kuona umuhimu wa elimu kwa watoto huku diwani wa kata hiyo ya Mtumbatu Amani Sewando akiahidi kushirikiana na viongozi wa kijiji hicho kutafuta wanafunzi ambao bado hawajaripoti shule hadi sasa.
Licha ya kutembelea shule hiyo ya sekondari Kitange Mbunge Prof. Kabudi amefanikiwa kukagua ujenzi wa shule ya sekondari Dumila ambapo ujenzi wake unagharimu takribani kiasi cha shilingi milioni 125 huku hadi sasa ikiwa imetumika kiasi cha zaidi ya milioni 123.