Prof Kabudi akabidhi mradi wa kukabarati barabara Kilosa
17 November 2023, 11:55 am
Serikali imeendelea kuwafikia wananchi waishio vijijini kwa kuwasogozea nyanja za ufunguzi wa maendeleo hususani katika ukarabati wa barabara kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini (TARURA) ambapo zinakwenda kuwaunganisha wananchi pamoja na kuwainua kiuchumi kwenye kilimo ambayo watayasafirisha hadi kwenye masoko ya kibiashara.
Na Asha Madohola
Wananchi wa kata za Maguha na Mamboya zilizopo wilayani Kilosa kwa muda mrefu walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya ubovu barabara hali iliyokuwa ikidhoretesha maendeleo ya vijiji vya Kife Maguha, Nyangala hadi Mamboya sasa wanakwenda kunufaika na ukarabati wa barabara ambao unatarajiwa kukamilika Juni 2024.
Akizungumza Meneja TARURA wilayani Kilosa Injinia Wiston Mnyaga katika makabidhiano ya utekelezaji wa mradi huo kwa Mhandisi wa mradi uliofanyika katika kata ya Maguha kijiji cha Nyangala na kuhudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Kilosa Mhe Prof Palamagamba Kabudi alisema kuwa mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 379 unasimamiwa na TARURA na kukamilika kwake utawasaidia wananchi kusafirisha mazao kutoka mashambani hadi kwenye masoko na kupata mahitaji muhimu ya kijamii.
“Ukarabati huu wa barabara hizi mbili unaenda kuondoa kero ya muda mrefu ya ubovu wa barabara na kuzifanya zipitike kipindi chote cha mwaka pamoja nakuinua pato la wananchi kwa kusafirisha mazao yao kutoka mashambani hadi kwenye masoko na serikali yetu sikivu imekuja na suluhisho la kudumu kwa kuzifanyia ukarabati wa barabara hizi kwa kuleta fedha” alisema Injinia Mnyaga.
Aidha Mhandisi Mnyaga aliwashukuru Rais Dkt Samia na Mbunge Prof Kabudi kwa kuona umuhimu wa kuleta fedha hizo ili kutatua kero ya barabara wataka viongozi wa kata, vijiji na wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi wa mradi huo hususan kwa wale watakaopatiwa kazi kuwa waaminifu na wadiilifu na kulinda vifaa ili kazi ilikusudiwa ikamilike na TARURA wapo tayari kuusimamia mradi huo.
Naye Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kilosa Bi Suzana Chayeka alimshukuru Rais kwa kufanya kazi za kuleta maendeleo kwa wananchi akishirikiana vyema na Mbunge Prof Kabudi ambaye amekuwa mstari wa mbele wa kutatua kero za wananchi hivyo wanatakiwa kuitunza miundombinu inayoletwa katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kilosa Mhe Prof Palamagamba Kabudi alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia kwa juhudi za kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi ambao wamekuwa wakikabiliwa na kero mbalimbali kama barabara na kwamba ukarabati wa barabara ya Nyangala hadi Mamboya ni fursa pekee ya utalii kwa kuwa barabara hiyo ni ya kihistoria wamisirionari wote walipita hapo.
Naye mkandarasi aliyekabidhiwa mradi huo wa ukarabati wa barabara wenye urefu wa kilomita 22.07 Injinia Joan Peter aliwaomba wananchi wa vijiji hivyo kumpatia ushirikiano kwenye ili aweze kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwamba ni wakati sahihi wa kuwapa ushirikiano viongozi ambao ndio wanaoletea maendeleo.
Awali wakizungumza baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo wameelezea adha wanayoipata kutokana na ubovu wa barabara iliyopo kwamba wazazi wanapata shida ya usafiri wanapokwenda kujifungua wengi wanafariki njiani hivyo wanamshukuru Rais na Mbunge kwa kuanza kuwatengenezea barabara.