Nguvu kazi za wananchi kuchochea miradi ya maendeleo kukamilika kwa wakati
30 May 2023, 2:57 pm
Miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita inadhamiria kuondoa adha za wananchi wanazokabiliana nazo ikiwemo katika sekta ya elimu, afya na masuala ya kijamii ambayo ili kukamilika inahitaji jitihada za wananchi kuunga mkono jitihada hizo hususan kujitolea nguvu kazi.
“Kipindi hiki tulichonacho ni cha serikali ya awamu ya sita ikiongozwa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan yapo mengi mazuri yaliyofanywa na serikali hii ni wajibu wetu kusimama naye imara ili miradi mingine iweze kutufikia”.
Na Asha Madohola
Wananchi wilayani Kilosa mkoani Morogoro wametakiwa kuwaunga mkono viongozi waliopo madarakani ili jitihada wanazofanya katika kuleta miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao ziweze kuleta matokeo chanya katika utekelezaji wake.
Hayo yalielezwa na viongozi teule ya ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof Palamagamba Kabudi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Mtumbatu iliyopo wilayani Kilosa ambapo walisema viongozi waliopo madarakani hususan ya awamu ya sita watumike kama tunu ya kuwaletea maendeleo bila kuangalia itikadi za rangi,dini,ukabila na siasa.
Akizungumza Katibu wa Mbunge Suzana Chayeka alisema kutokana na juhudi zinazofanywa na viongozi za kuleta maendeleo wilayani kote ofisi yake itakua mstari wa mbele wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi hivyo aliwataka wafike ofisini ili waweze kutatua changamoto kwa pamoja.
Naye Msaidizi wa Katibu kutoka Ofisi ya Mbunge Yahaya Konala alisema serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepiga hatuka kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi hivyo ni jukumu lao kuhakikisha linaunga mkono jitihada hizo na katika nafasi ya Mbunge Prof Kabudi yupo tayari kuwaletea maendeleo wananchi wa Mtumbatu na kwamba sio wakati sahihi wa kusikiliza maneno yenye nia ovu ya kuwapoteza.
“Wananchi wa jimbo la Kilosa tujivunie uwepo wa kiongozi wetu Mbunge Prof Palamagamba Kabudi aliyetuheshimisha Kilosa na kutufanya tutembee vifua mbele kutokana uadilifu aliounesha kwa Mhe Rais ndio mana miradi inakuja katika maeneo yetu” alisema Konala.
Kwa upande wake Msimamizi wa kitengo cha Habari na Uhamasishaji mitandaoni kutoka ofisi ya Mbunge, Mkude Mussa Magathi alisema kuwa Mbunge wa jimbo la Kilosa Prof Palamagamba Kabudi amehakikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwepo ujenzi wa kituo cha afya wenye thamani ya Shilingi milioni 900, ujenzi wa daraja la Berega wenye thamani ya Shilingi bilion saba hizo ni jitihada za Mbunge wa jimbo la Kilosa hivyo wananchi wanapaswa wamuunge mkono kiongozi huyo ambaye anapambana kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Mtumbatu Mhe Amani Sewando alimshukuru Mhe mbunge wa jimbo la Kilosa kwa kuwasaidia kuwaletea mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi kupitia mradi wa Boost ambapo katika shule ya Mtumbatu yenye wanafunzi 1724 wanasoma kwa kurundikana katika madarasa tisa yaliyopo ambayo manne ni chakavu hivyo ombi lake lilikua ni kujengewa madarasa na kwa mwaka huu fedha ujenzi wa shule mpya wenye madarasa saba na majengo ya utawala umeshaanza na ameahidi anausimamia vema ili ukamilike kwa wakati.