FM Manyara
FM Manyara
12 February 2026, 4:37 pm

Shirika la SO THEY CAN Tanzania limesema kwa mwaka huu wa 2026 linatarajia kupanua wigo wake kwa mkoa wa Manyara ili kufikia maeneo mengine yenye changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi huku bajeti yao ikiongezeka mwaka hadi mwaka tangu kuanza kufanya kazi katika halmashauri ya wilaya ya Babati.
Na Marino Kawishe
Akizungumzia dira ya Shirika kwa miaka mitano ijayo 2026-2030 kwenye mkutano wa mwaka wa wadau wa Shirika hilo, meneja mkazi wa STC Roselyne Mariki amesema kwa zaidi ya miaka kumi wamefanya miradi mbali mbali kwenye sekta ya miundo mbinu ya elimu kwenye ukanda wa Galapo na sasa ni wakati wakujitanua zaidi kwenye mikoa mingine miwili.
Aidha ameainisha maeneo ambayo waliyafanyia kazi kwa miaka 10 iliyopita kuwa ni pamoja na ujenzi wa chuo cha ualimu Mamire, ujenzi wa madarasa, vyoo vya waalimu na wanafunzi , mafunzo kwa wazazi mahiri pamoja na kuendesha kambi za afya kwenye maeneo ya miradi ya Shirika.
Kwa upande wake mgeni rasmi kwenye mkutano huo ambae ni mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Babati Anna Mbogo ameitaka jamii kuendelea kutoa ushirikiano zaidi na kushiriki kikamilifu kufanikisha miradi hiyo.
Aidha kwa miaka mitano ijayo Shirika hilo linatarajia kutoa mafunzo kwa waalimu na kamati za shule, kuendeleza miradi ya kilimo, kambi za afya ambazo zitafanyika mara mbili kwa mwaka pamoja na uanzishaji na ukuzaji wa vikundi vya kuweka na kukopa kwenye maeneo ya mradi wa shirika hilo.
