FM Manyara
FM Manyara
12 September 2025, 10:32 am

Na Marino Kawishe
Mgombea ubunge kwa tiketi ya chama cha mapinduzi ( CCM) jimbo la Babati Vijijini Daniel Baran Sillo amewataka wananchi wa jimbo la Babati Vijijini kumchagua Rais Dr Samia Suluh Hassan kwenye uchaguzi utakaofanyika tarehe 29 october mwaka huu.
Akizungumza mbele ya wananchi wa kata ya Mamire waliohudhuria ufunguzi wa kampeni zake amesema vipaumbele vyake atakapopata nafasi yakuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa awamu nyingine ni kuhakikisha miundo mbinu ya barabara, elimu, upatikanaji wa maji safi na salama na huduma za afya ambayo ilishaanza wakati akiwa mbunge inakamilika ili kutatua kero kwa wananchi wa jimbo lake.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi kwenye uzinduzi wa kampeni hizo ambaye ni mjumbe wa mkutano Mkuu CCM Taifa Joachim Muungano amemuomba aliyekuwa Diwani wa kata ya Mamire Tarmo Kurudi ndani ya chama chake cha CCM ili kukamilisha kwa pamoja miradi ambayo ilishaanzishwa wakati akiwa Diwani wa kata hiyo
Aidha aliyekuwa mtia nia wa kuwania ubunge katika jimbo la Babati Vijijini Emanuel Philip Gekul ambaye hakufanikiwa kuchaguliwa wakati wa kura za maoni amewataka Wana CCM kutokuwa na Makundi na badala yake kumuunga mkono Daniel Sillo pamoja na madiwani waliopitishwa kwa tiketi ya CCM kwenye uchaguzi ujao.
Katika ufunguzi huo wa Kampeni za mgombea ubunge wa jimbo la Babati Vijijini zimehudhuriwa na wagombea udiwani wote wa kata 25 pamoja na Baadhi ya wagombea wa nafasi ya ubunge akiwemo Asia Halamga kutoka Hanang na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara Regina Ndege.