FM Manyara
FM Manyara
21 June 2025, 10:41 pm

Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (EWURA) kanda ya kaskazini imekutana na wadau wa nishati ya gesi ambao ni wasambazaji na wauzaji wa mitungi ya gesi ya kupikia majumbani (LPG) mkoani manyara na kuwapa elimu, kanuni na miongozo ya ufanyaji wa biashara hiyo ili waweze kufanya biashara zao kwa kuzingatia misingi na taratibu za kisheria na kutofungiwa leseni zao.
Akizungumza leo meneja wa EWURA kanda ya kaskazini Mhandisi Lorivii Long’idu katika semina waliyoiandaa na kufanyika katika ukumbi wa White rose mjini Babati amesema lengo la semina hiyo ni kuwakumbusha wafanyabiashara hao majukumu yao, namna ya kupata leseni pamoja na kuwasisitiza utaratibu wa kufanya biashara hiyo.
Aidha Mhandisi long’idu amesema kwa sasa matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi ya kupikia majumbani (LPG) kwa wananchi imekuwa kwa asilimia kubwa na wao kama EWURA wanaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo ili kufikia lengo la serikali ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa chama cha waingizaji na wasambazaji wa gesi za kupikia majumbani (LPG) Mhandisi Amos Jackson Mwansumbule amesema elimu iliyotolewa na EWURA kwa wafanya biashara hao ni nzuri kwakuwa inawasaidia kuepukana na majanga katika biashara zao na pia kwa watumiaji wa mwisho wa gesi hizo .
Nao baadhi ya wafanyabiashara na wasambazaji wa mitungi ya gesi za kupikia wameishukuru EWURA kwa kuwapatia elimu muhimu na kuomba mamlaka hiyo pia iweze kudhibiti na kutatua changamoto zinazoikumba biashara hiyo ikiwemo ujazaji holela wa mitungi ya gesi inayosababisha kuondoa uaminifu kwa wateja wao.