FM Manyara
FM Manyara
8 May 2025, 5:51 pm

Na Mzidalifa Zaid
Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Maryam Ahmed Muhaji ameitaka jamii kuunganisha nguvu za pamoja katika kusaidia wasichana shuleni ili kupata taulo za kike katika kustawisha hedhi salama na kufanya vizuri katika masomo yao.
Muhaji ameyasema wilayani Babati mkoani Manyara wakati wa mafunzo kwa baadhi ya wanafunzi na walimu pamoja na wadau wengine wa Afya mkoani Manyara na ngazi ya taifa kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya taulo za kike na utambulisho wa mradi wa usambazaji wa taulo za kike kutoka Kampuni ya Real Relief kupitia mradi wa SAFEPAD na kampuni ya A to Z.
Kwa upande wake Afisa Programu kutoka Mpango wa Taifa wa Afya na Lishe Shuleni , Wizara ya Afya Dkt. Julietha Tibyesiga amesema hedhi salama inapozingatiwa ni namna bora ya kumtunza msichana shuleni ili aweze kusoma vizuri na akizungumzia Maandalizi ya Mwongozo wa Usimamizi wa Hedhi salama.
Katibu wa Jukwaa la Hedhi Salama Tanzania Severine Allute na Irine Maganga kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wamesema mradi wa SAFEPAD utarahisisha wanafunzi kuwa na mazingira safi na salama na kuwezesha kujifunza kwa ufasaha na mradi huo utarahisisha Mkoa wa Manyara kuwa na upatikanaji wa taulo za kike.
Nao baadhi ya wanafunzi wanufaika wamradi huo akiwemo Zaina Khatibu kutoka shule ya Sekondari Babati Day pamoja na Anna Bahati kutoka shule ya Msingi Komoto wamesema suala la hedhi salama lina mchango mkubwa katika kupunguza utoro shuleni na wakishukuru mafunzo yaliyotolewa kupitia mradi huo.
